WIRE โ€” SIKU chache zilizopita, baadhi ya shule jijini Nairobi zilionya wazazi kuhusu visa vinavyoshukiwa kuwa vya matumbwitumbwi (mumps), ugonjwa unaoambukiza na kuenea kwa urahisi miongoni mwa watoto. Tahadhari hizo zimezua wasiwasi miongoni mwa wazazi huku shule zikiwataka kufuatilia watoto wao kwa dalili kama homa, uchovu na kuvimba kwa tezi za kutengeneza mate kwenye koo au chini na mbele ya masikio. Dkt Varsha Vekaria-Hirani, daktari bingwa wa watoto, anaeleza kuwa mazingira ya shule yanaweza kuchangia kuenea kwa ugonjwa huo kwa sababu ya msongamano wa wanafunzi, ukaribu wa watoto na tabia ya kushirikiana chakula na chupa za maji. Matumbwitumbwi ni maambukizi ya virusi yanayoathiri tezi za kutengeneza mate (parotid glands), almaarufu kama findofindo zinazopatikana kwenye koo na mbele ya masikio na ambazo hutoa mate wakati mtu anapotafuna chakula. "Matumbwitumbwi husababishwa na virusi ambavyo huenea sana hasa pale ambapo kuna msongamano. Kwa kawaida mlipuko wake huwa ya msimu," anaeleza Dkt Vekaria-Hirani. Anasema ugonjwa huo huenea kupitia matone ya hewa yanayotolewa na mtu aliyeambukizwa anapokohoa au kupiga chafya. Mtu aliyeambukizwa anaweza pia kueneza virusi hivyo kupitia mate. "Msongamano wa wanafunzi madarasani na watoto kushirikiana chakula au chupa za maji shuleni huenda zikachangia kuenea kwa matumbwitumbwi," alisema. Hata hivyo, hakuna data rasmi ya kitaifa inayoonyesha ongezeko la visa vya matumbwitumbwi nchini. Dkt Vekaria-Hirani anaeleza kuwa ingawa visa vimeripotiwa na baadhi ya shule, hasa Nairobi, na wahudumu wa afya wamekuwa wakiwaona watoto wenye ugonjwa huo mara kwa mara, takwimu rasmi za kitaifa hazipatikani.Mombasa pia imetajwa miongoni mwa maeneo ambako visa vimeripotiwa. "Kwa sasa hakuna data rasmi ya kitaifa, lakini baadhi ya shule zimeripoti ongezeko la visa na sisi kama wahudumu wa afya tumekuwa tukiwaona watoto wenye matumbwitumbwi mara kwa mara," alisema. Watoto walio chini ya miaka 15, hasa wanaokwenda shule, wanaonekana kuwa miongoni mwa walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa. Dalili za awali Dkt Vekaria-Hirani anaeleza kuwa matumbwitumbwi huanza kwa dalili zinazoweza kufanana na mafua au maambukizi mengine ya virusi. Katika siku tatu au nne za kwanza, mtoto anaweza kupata homa, udhaifu, maumivu ya misuli, uchovu na kukosa hamu ya kula. Baadaye, tezi ya kuunda mate inaweza kuanza kuvimba upande mmoja au pande zote mbili. Uvimbe huo kwa kawaida huambatana na maumivu ambayo huongezeka mtoto anapotafuna chakula. Vyakula vyenye uchachu vinaweza kufanya maumivu kuwa makali zaidi kwa sababu huchochea uzalishaji wa mate. "Wazazi wanapaswa kuangalia homa, uchovu, kukosa hamu ya kula na baadaye uvimbe wenye maumivu chini au mbele ya masikio," alisema. Hata hivyo, si kila uvimbe katika eneo hilo ni matumbwitumbwi. Maambukizi ya koo kama tonsils na pharyngitis yanaweza pia kusababisha kuvimba kwa tezi hizo. Kinachofanya matumbwitumbwi kuwa vigumu kudhibiti ni kwamba mtoto anaweza kuwaambukiza wengine kabla ya wazazi kutambua kuwa ana ugonjwa huo. Dkt Vekaria-Hirani anasema mtu aliyeambukizwa anaweza kuanza kueneza virusi siku moja au mbili kabla ya kuvimba kwa tezi za kutengeneza mate. Mtoto anaweza kuendelea kuwa mwenye uwezo wa kuambukiza wengine kwa takriban siku tano baada ya kuanza kwa uvimbe. Hii ina maana kuwa mtoto anaweza kwenda shuleni akiwa na homa kidogo, uchovu au kukosa hamu ya kula bila wazazi kujua kuwa tayari anaweza kuwaambukiza wengine. Kipindi cha mtu kuambukizwa hadi kuanza kuonyesha dalili kinaweza kuwa kati ya wiki mbili na tatu. Dkt Vekaria-Hirani anawashauri wazazi kuwaruhusu watoto wanaoshukiwa kuwa na matumbwitumbwi kukaa nyumbani na kuepuka kuwapeleka shuleni au kutangamana na watoto wengine. Anasema mtoto anapaswa kubaki nyumbani kwa siku tano baada ya kuanza kuonyesha dalili za kuwa na findofindo kooni. Wazazi pia wanapaswa kuijulisha shule ili hatua za kuzuia maambukizi zichukuliwe. "Mtoto anapaswa kubaki nyumbani kwa siku tano, shule ijulishwe na mtoto aonekane na daktari ili achunguzwe iwapo kuna matatizo mengine," alisema. Kwa matumbwitumbwi yasiyo na madhara mengine, matibabu hulenga kudhibiti dalili kama homa na maumivu. Dkt Vekaria-Hirani alisema antibiotiki hazitibu ugonjwa huo kwa sababu unasababishwa na virusi, wala si bakteria. Ingawa watoto wengi hupona bila kupata changamoto, matumbwitumbwi yanaweza kusababisha madhara mengine. Miongoni mwa matatizo hayo ni kuvimba kwa korodani kwa wavulana, hali inayojulikana kama orchitis, na uvimbe wa ovary kwa wasichana. Ugonjwa huo pia unaweza kusababisha maambukizi au uvimbe wa ubongo, ikiwemo meningitis na encephalitis. Baadhi ya wagonjwa wanaweza pia kupoteza uwezo wa kusikia au kupata uvimbe wa kongosho, unaojulikana kama pancreatitis. Dkt Vekaria-Hirani anawashauri wazazi kutafuta matibabu ya haraka mtoto anapopata maumivu ya korodani, maumivu makali ya tumbo, kuchanganyikiwa, maumivu makali ya kichwa au kutapika. Dkt Vekaria-Hirani alisema chanjo dhidi ya matumbwitumbwi kwa sasa haijajumuishwa katika ratiba ya kawaida ya chanjo za KEPI nchini Kenya. Hii inamaanisha kuwa watoto wengi hawana kinga maalumu dhidi ya ugonjwa huo. Familia pia zinashauriwa kunawa mikono mara kwa mara, kutoshirikiana chakula au chupa za maji na watu wengine na kusafisha sehemu zinazoguswa mara kwa mara. Watoto wafundishwe pia kufunika mdomo wanapokohoa au kupiga chafya. Dkt Vekaria-Hirani alisema baadhi ya wazazi wanaamini kimakosa kuwa matumbwitumbwi yanahitaji antibiotiki. Wengine huamini kuwa kila mvulana au msichana anayeugua ugonjwa huo atakuwa tasa. Kwa sasa, wazazi wanahimizwa kuwa macho kwa dalili za ugonjwa huo na kutafuta ushauri wa daktari mapema ili kupunguza hatari ya maambukizi kuenea shuleni na katika jamii.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.