WIRE โ ALIYEKUWA Gavana wa Migori Okoth Obado, amepatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno, aliyekuwa mjamzito. Aliyekuwa msaidizi wake wa kibinafsi Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa Kaunti ya Migori Caspal Obiero pia walipatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi huyo. Jaji Cecilia Githua wa Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi alisema upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka kuwa watatu hao walishirikiana kupanga na kutekeleza mauaji ya Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26 na ujauzito wa wiki 28 alipouawa mwezi Septemba 2018. Mahakama ilisema Sharon alitekwa nyara, akabakwa na baadaye kuuawa ili kuzuia uhusiano wake na Obado pamoja na ujauzito wake usijulikane kwa umma. "Nimeridhika kuwa ushahidi uliowasilishwa unaonyesha msururu kamili wa matukio usioacha shaka kwamba washtakiwa walishirikiana na watu wengine ambao hawako mahakamani kutekeleza mauaji hayo. Ushahidi unaonyesha wazi kwamba walisababisha kifo cha Sharon," alisema Jaji Githua. Kwa mujibu wa mahakama, Obado ndiye aliyekuwa na sababu ya kutaka Sharon auawe, akitoa fedha na kuchochea mpango huo huku Oyamo akisaidia utekelezaji wake na Obiero akitoa usaidizi wa kimipango na kusaidia kuficha uhalifu huo. Mahakama ilisema majukumu ya kila mmoja yalionyesha maandalizi ya makusudi,ย ushiriki wao na juhudi za kuficha mauaji hayo. "Hivyo basi, ninapata kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu bila shaka yoyote," alisema jaji. Hukumu hiyo inahitimisha kesi iliyodumu kwa karibu miaka saba. Kesi hiyo ilicheleweshaย kutokana na maombi 16 ya kisheria, kuhamishwa kwa jaji aliyekuwa akiisikiliza baada ya mashahidi 25 kutoa ushahidi, pamoja na kusimamishwa kwa kesi kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya Jaji Mkuu kuagiza isikizwe tena. Kwa jumla, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 42 kuthibitisha kesi yake. Mahakama ilitupilia mbali utetezi wa Obado kwamba alikuwa amekubali ujauzito huo na kuendelea kumsaidia Sharon kifedha. Jaji Githua alisema ingawa Obado alikiri kujua kuhusu ujauzito huo mwezi Machi 2018, baadaye alianza kumuepuka Sharon, akasitisha msaada wa kifedha na kujaribu kuzuia uhusiano wao usijulikane hadharani. "Si jambo la bahati mbaya kwamba alianza kuwa na wasiwasi mara tu ilipoonekana kuwa habari hizo zingechapishwa. Ni wazi alitaka kuzuia suala hilo lisifikie umma," alisema jaji. Mahakama ilisema Sharon alikuwa akimtaka Obado akubali hadharani kuwa mimba ilikuwa yake, amnunulie nyumba na gari, pamoja na kumtafutia kazi. Alidai kuwa angeweka wazi uhusiano wao iwapo madai hayo yasingetimizwa. Jaji alikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka kwamba fedha ambazo Sharon alipokea kupitia Oyamo hazikuwa za kumsaidia, bali zilikuwa sehemu ya njama za kumshawishi aachane na mpango wa kufichua siri hiyo huku maandalizi ya kumuua yakiendelea. Ushahidi wa rafiki wa karibu wa Sharon ulionyesha kuwa Obado alimpa Sh30,000 ili atoe mimba na akamwelekeza awasiliane na Oyamo kuhusu masuala yote yaliyohusu ujauzito huo. Shahidi huyo pia alisema Sharon alikuwa amemchezea rekodi za sauti za mazungumzo yake na Obado, ambapo alikuwa akimsihi asichapishe picha zao kwenye mitandao ya kijamii na kumshawishi mara kwa mara kutoa mimba akisema muda ulikuwa ukiisha. Mahakama pia ilitegemea ushahidi wa rafiki wa familia kwa jina Lawrence aliyejaribu kupatanisha wawili hao baada ya Obado kukubali kuwa alijua kuhusu ujauzito huo. Kwa mujibu wa ushahidi huo, Obado alimwahidi Sharon kuwa angemnunulia shamba na kumjengea nyumba iwapo angeacha kufichua uhusiano wao. Hata hivyo, Jaji Githua alisema ahadi hizo hazikuwa za dhati bali zilikuwa mbinu ya kununua muda huku mpango wa kumuondoa Sharon ukiendelea kutekelezwa. Kwa hukumu hiyo, watatu hao sasa wanasubiri mahakama kutangaza adhabu watakayopatiwa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mwanafunzi huyo, kesi ambayo ilivuta hisia za taifa kwa miaka kadhaa. Jana, Mahakama ilifuta dhamana ya watatu hao, wakazuiliwa rumande hadi Agosti 18 kusubiri ripoti ya kabla ya kuhukumiwa.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.