WIRE — TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imesema inawafuatilia wanasiasa wanaotumia mamilioni ya pesa katika hafla za uwezeshaji wa wananchi, ikionya kuwa mali waliyotangaza inaweza kufichua iwapo fedha hizo zinatokana na vyanzo halali. Tume hiyo ilisema kutoa fedha taslimu katika mikutano ya kisiasa kumeibua maswali kuhusu iwapo baadhi ya viongozi wanaishi zaidi ya kipato chao kinachojulikana. Katika miezi ya hivi majuzi, viongozi wa upinzani, viongozi wa kidini na wanaharakati wamekuwa wakitaka serikali ichunguze chanzo cha fedha zinazotolewa katika hafla hizo. Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud alisema maafisa wa umma hulazimika kutangaza mali, mapato na madeni yao kila baada ya miaka miwili, jambo litakalowezesha tume kulinganisha mali waliyotangaza na kiasi cha fedha wanachogawa hadharani. "Maafisa wa umma wanatakiwa kutangaza mali yao kila baada ya miaka miwili. Tukigundua kuwa kuna mali ambayo hawawezi kueleza ilivyopatikana, tunafanya uchunguzi na kuwasilisha suala hilo mahakamani ili iamue iwapo ilipatikana kinyume cha sheria," alisema Bw Mohamud. Alizungumza Kisumu Jumanne wakati EACC ilipotangaza kuanza mchakato wa kurejesha ardhi ya Huduma ya Magereza ya Kenya yenye thamani ya Sh4.3 bilioni inayodaiwa kutwaliwa isivyo halali. Bw Mohamud alisema tume ilitoa notisi mnamo Novemba 12, 2025 ikiwataka maafisa wa umma kutangaza mapato, mali na madeni chini ya Sheria ya Migongano ya Maslahi ya mwaka 2025. Kwa mujibu wa notisi hiyo,  tangazo hili lilipaswa kuwasilishwa kati ya Novemba 1 na Desemba 31, 2025. EACC pia inatarajiwa kuwataka baadhi ya wanasiasa kueleza chanzo cha fedha wanazotumia katika shughuli hizo na kubaini iwapo ni misaada ya kawaida, kampeni za kisiasa au matumizi mabaya ya nyadhifa za umma. Hata hivyo, Bw Mohamud alisema kubeba fedha taslimu si kosa la jinai. "Kuwa na pesa si kosa. Swali ni, fedha hizo zimetoka wapi? Je, ni matokeo ya uhalifu au zinanuiwa kutoa hongo? Ni lazima fedha zihusishwe na uhalifu kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa," alisema. Katika miezi ya hivi majuzi, viongozi wengi hasa wanaounga mkono serikali jumuishi wamekuwa wakifanya hafla za uwezeshaji katika maeneo mbalimbali wakitoa mamilioni ya fedha. Mfano mmoja ni hafla iliyofanyika Suna Mashariki, ambapo Mbunge Junet Mohamed alitoa Sh10 milioni akiwa amebeba kwenye mkoba mgongoni, huku Rais William Ruto naye akichangia Sh10 milioni. Kwa mujibu wa taarifa za mishahara ya viongozi wa umma, mbunge hupokea mshahara na marupurupu yanayofikia takriban Sh1.45 milioni kwa mwezi.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.