WIRE โ KWA takriban miongo mitatu, aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga alijijengea jina kama kinara wa siasa za upinzani nchini. Alitumia mbinu mbalimbali kama kususia bidhaa, kuhamasisha wananchi kupitia mikutano ya kisiasa, kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa na kuunda miungano ya kisiasa ili kuongeza presha kwa serikali zilizokuwa mamlakani. Sasa, chini ya miaka miwili tangu atofautiane na Rais William Ruto, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anaonekana kufuata mkondo huo huo aliokuwa akiukosoa vikali alipokuwa serikalini. Kauli yake ya kuwashauri watalii na wawekezaji wa kigeni wasubiri hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 kabla ya kuja Kenya inachukuliwa na wachambuzi kama ishara kwamba sasa amekumbatia mbinu za jadi za upinzani. Kama alivyofanya Raila kwa miaka mingi, Bw Gachagua sasa anatumia shinikizo za kiuchumi, ujumbe kwa jamii ya kimataifa na siasa za miungano kujaribu kushinikiza serikali bila kuwa mamlakani. Mfanano mkubwa zaidi kati ya viongozi hao wawili ni matumizi ya uchumi kama silaha ya kisiasa. Mwaka 2017 na baadaye 2023, Raila aliwataka Wakenya kususia bidhaa na huduma za kampuni alizodai zinaunga mkono serikali. Wakati huo, Bw Gachagua akiwa Naibu Rais alimshutumu Raila kwa kuharibu biashara na kuhatarisha ajira. Lakini sasa, Bw Gachagua ameenda hatua zaidi kwa kuwashauri watalii na wawekezaji wa kigeni waahirishe safari na uwekezaji wao nchini akidai hali ya usalama imezorota. Kauli hiyo imeibua ukosoaji mkubwa, si kutoka kwa serikali pekee bali pia ndani ya muungano wa upinzani. Msemaji wa Muungano wa Upinzani Dkt Mukhisa Kituyi alisema hakubaliani na wito wowote unaoweza kudhoofisha sekta muhimu ya utalii, akisema kuna njia nyingine za kukosoa serikali bila kuathiri uchumi. Mbinu nyingine ambayo Raila alitumia kwa miaka mingi ilikuwa kupeleka malalamishi ya kisiasa ya Kenya katika jukwaa la kimataifa. Baada ya uchaguzi tata na wakati wa misukosuko ya kisiasa, Raila mara kwa mara alikutana na mabalozi na jamii ya kimataifa kueleza changamoto za utawala na demokrasia. Bw Gachagua naye sasa anaonekana kufuata njia hiyo kwa kutumia majukwaa ya kimataifa kueleza madai ya ukosefu wa usalama, ukiukaji wa haki za kisiasa na matumizi mabaya ya mamlaka. Aidha, kama Raila, Bw Gachagua amejikita katika kujenga muungano mpana wa kisiasa. Mbali na viongozi wa Muungano wa Upinzani kama Kalonzo Musyoka, Dkt Fred Matiang'i, Martha Karua, Justin Muturi na Eugene Wamalwa, amekuwa akifanya mikutano na kiongozi wa Safina Jimi Wanjigi nyumbani kwake Wamunyoro. Lengo ni kuunganisha viongozi kutoka maeneo mbalimbali ili kutoa changamoto kubwa kwa serikali ya Kenya Kwanza. Kama Raila alivyoanza kwa kuimarisha ngome yake ya Nyanza kabla ya kupanua ushawishi wake, Bw Gachagua naye ameanza kwa kuimarisha uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya kabla ya kuelekea Ukambani, Magharibi na Pwani.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.