WIRE โ POLISI katika Kaunti ya Mombasa wanamzuilia mwanamume aliyepatikana amemeza madonge ya dawa za kulevya, akilenga kuyasafirisha hadi Dubai yakiwa ndani ya mwili wake. Mnamo Julai 15, wakati wasafiri wakisubiri kuabiri ndege ya saa saba mchana kutoka Mombasa kuelekea Dubai, wapelelezi katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi jijini Mombasa walikuwa wakimfuatilia mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 67. Taarifa za kijasusi zilikuwa zimemhusisha na mtandao wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya, huku wachunguzi wakishuku kwamba alikuwa ameficha kokeini ndani ya mwili wake. Wapelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), wakishirikiana na maafisa wa usalama wa uwanja huo wa ndege, walimkamata kabla ya kuabiri ndege. Operesheni hiyo baadaye ilihusishwa na mtandao wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya ambao umekuwa ukichunguzwa kwa miezi kadhaa. [caption id="attachment_190364" align="alignnone" width="2560"] Polisi wapata mihadarati kutoka kwa msafiri mmoja aliyekuwa anaelekea Dubai Picha|Kevin Odit[/caption] Walanguzi hao wa kimataifa hutumia Mombasa kama kituo cha kupitisha dawa za kulevya kuelekea nchi nyingine za nje. Mshukiwa alikamatwa na kupelekwa katika kituo maalumu cha kutengwa kwa ajili ya uangalizi wa kimatibabu. Baadaye alipelekwa katika Hospitali ya Port Reitz, ambapo madaktari na wahudumu wa afya walimweka chini ya uangalizi wa karibu ili kusaidia kutoa dawa hizo alizokuwa amemeza kwa njia salama. Polisi walisema wataalamu wa matibabu walifanikiwa kutoa vidonge 44 vilivyofunikwa kutoka tumboni mwake kwa njia iliyolenga kuvizuia kupasuka. "Dawa hizo za kulevya zitatumika kama vielelezo mahakamani," alisema Kamanda wa Polisi wa eneo la Pwani Ali Nuno. Kulingana na wachunguzi, kumeza dawa za kulevya ili kukwepa ukaguzi wa usalama ni mojawapo ya njia hatari zaidi za kusafirisha dawa hizo, kwa sababu vikipasuka ndani ya mwili vinaweza kusababisha maafa. Polisi walifichua kwamba kukamatwa kwa mwanamume huyo kulitokana na operesheni inayoendelea ambayo hadi sasa imesababisha kukamatwa kwa washukiwa wengine kadhaa, wakiwemo wanaodaiwa kuwa walanguzi wakuu wa dawa za kulevya. Kwa jumla, dawa za kulevya zenye thamani ya karibu Sh151 milioni zimepatikana na polisi katika kipindi cha karibu miezi minne iliyopita. Operesheni hiyo pia ilifanikisha kukamatwa kwa mshukiwa mwingine ambaye wapelelezi wanaamini alikuwa kinara wa biashara hiyo haramu. Wakati wakiendeleza uchunguzi, maafisa walivamia nyumba iliyoshukiwa kutumiwa kama maficho na kituo cha muda cha kuwahifadhi wasafirishaji wa dawa za kulevya. Upekuzi huo ulisababisha kupatikana kwa vipande vingine 16 vinavyodhaniwa kuwa na kokeini. Uchunguzi unaendelea kubaini ukubwa kamili wa mtandao huo na kuwatambua washukiwa wengine. Takwimu zilizotolewa na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha DCI zinaonyesha kwamba wapelelezi wamekamata kilo 37 za heroini zenye thamani ya takriban Sh111.846 milioni katika miezi minne iliyopita. Pia wamekamata gramu 1,336 za kokeini zenye thamani ya takriban Sh5.344 milioni. "Jumla ya watu tuliowakamata kuhusiana na dawa za kulevya ni washukiwa 27. Kati yao, watano ni wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya bila shaka yoyote, 10 ni wasafirishaji na 12 ni wauzaji," alisema Bw Nuno. Ripoti hiyo pia inaonyesha kwamba maafisa walikamata gramu 204 za methamphetamine, inayofahamika zaidi kama meth, yenye thamani ya takriban Sh1.632 milioni katika operesheni zilizofanywa katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Bangi bado ndiyo dawa ya kulevya inayokamatwa zaidi katika eneo hilo, polisi wakiripoti kukamata kilo 10,747.84 zenye thamani ya takriban Sh32.243 milioni katika kipindi hicho. Kwa jumla, thamani ya dawa zote za kulevya zilizokamatwa katika operesheni za kupambana na biashara hiyo katika eneo la Pwani ni takriban Sh151.065 milioni.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.