WIRE โ€” TANGAZO la Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwa atawania urais mnamo 2027 linaendelea kubadili mwelekeo wa siasa za upinzani na ODM, huku viongozi wengi wakianza kujiunga na mrengo wa Linda Mwananchi anaouongoza. Akizungumza katika mikutano ya kisiasa Kaunti ya Taita Taveta mwishoni mwa wiki, Bw Sifuna alisema licha ya kupokonywa nyadhifa za ukatibu mkuu wa ODM na kiranja wa wachache, anaamini vijana watampa nafasi ya kuwa rais 2027. "Wameninyang'anya kila cheo nilichopewa na Baba, lakini vijana wanasema watanipa cheo cha H.E," akasema. Miongoni mwa viongozi ambao wamebadili msimamo ni Seneta wa Kisii Richard Onyonka, ambaye awali alikuwa mshirika wa karibu wa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i. Bw Onyonka ameonekana mara kadhaa katika mikutano ya Linda Mwananchi na hadharani ameahidi kumuunga mkono Bw Sifuna ikiwa atawania urais. "Mdogo wangu na rais ajaye ni Edwin Sifuna. Ukifika wakati wa kupiga kura nitampigia kura. Nawaona wengine wanatetereka nikisema hivyo lakini sote katika upinzani tuko pamoja," akasema akiwa Voi. Bw Onyonka alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa mstari wa mbele kumpigia debe Dkt Matiang'i alipozindua azma yake ya urais mnamo 2025. Hata hivyo, hakuhudhuria ziara ya Dkt Matiang'i huko Keumbu, ambako wafuasi wa Linda Mwananchi walivamiwa. Viongozi wengine wa Gusii wanaohusishwa na mrengo huo ni wabunge Clive Gisairo, Anthony Kibagendi na Obadiah Barongo. Ndani ya ODM, mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang' walitumia matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ol Kalou kuikosoa serikali, wakisema viongozi wanapaswa kuwasikiza wananchi na kuheshimu maamuzi yao badala ya kutumia vitisho au rushwa. Kauli zao zimezua hisia kwamba wanaegemea upande wa Linda Mwananchi, ingawa hawajatangaza rasmi msimamo wao. Wakati huo huo, Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata alikosolewa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kumuunga mkono mgombea wa Linda Mwananchi katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Mchanganuzi wa masuala ya siasa Martin Andati anasema hatua hiyo ilionyesha kuwa siasa za eneo la Mlima Kenya zinaendelea kubadilika, huku viongozi wakitafuta miungano mipya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Shinikizo pia zinaongezeka kwa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, huku baadhi ya wabunge wa Ukambani wakihusishwa na shughuli za Linda Mwananchi. Duru hata hivyo zinaashiria kuwa lengo la wabunge hao ni kuhakikisha Mabw Kalonzo na Sifuna wanashirikiana katika uchaguzi wa 2027. Miongoni mwa wabunge wa Wiper wanaohusishwa na mrengo huo ni Joshua Kimilu, Patrick Makau na Danson Mwashako. Katika Magharibi mwa Kenya, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anaendelea kushirikiana na Linda Mwananchi na anapanga mikutano ya kisiasa Trans Nzoia na Bungoma. Ni katika mikutano hiyo ambapo Bw Sifuna anatarajiwa kutawazwa kuwa kigogo wa siasa za Magharibi na kupewa baraka za kuwania urais.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.