WIRE โ FAMILIA ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga leo itakabidhi serikali sehemu ya kujenga kaburi la heshima la mwanasiasa huyo mashuhuri wa upinzani. Hafla hiyo itafanyika Kang'o ka Jaramogi, Bondo, Kaunti ya Siaya. Wakati huo huo, mwanawe marehemu, Raila Odinga Junior ameanza kuweka msingi wa kuingia katika siasa za uchaguzi huku akilenga kuwania kiti cha ubunge cha Embakasi Kusini katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Jumapili, Raila Junior alikutana na kiongozi wa ODM ambaye pia ni ami yake , Dkt Oburu Oginga, ambapo walijadili maandalizi ya ujenzi wa kaburi hilo pamoja na siasa. Katika mahojiano na Taifa Leo, Raila Junior alisema mazungumzo yao yalihusu masuala mbalimbali ya kifamilia, huku sherehe ya kukabidhi eneo hilo kwa serikali ikiwa ajenda kuu. Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Ummi Bashir, Gavana wa Siaya James Orengo, wanafamilia, ukoo wa Kawuor pamoja na wakazi wa Bondo wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo katika Kang'o ka Jaramogi, ambako mwili wa Raila ulizikwa. Hafla hiyo itakuwa ya kwanza kwa Dkt Oginga na Gavana Orengo kushiriki jukwaa moja tangu kuzuka kwa mgawanyiko ndani ya ODM kuhusu uongozi wa chama. Gavana Orengo anahusishwa na mrengo wa Linda Mwananchi na amekuwa akijitambulisha kama kiongozi halali wa ODM. Kaburi la heshima la Raila litajengwa karibu na lile la babake, aliyekuwa Makamu wa Rais Jaramogi Oginga Odinga, aliyefariki Januari 20, 1994. Jaramogi alikuwa miongoni mwa vinara waliopigania mfumo wa vyama vingi nchini na aligombea urais mnamo 1992, akimaliza katika nafasi ya nne. Raila Junior, ambaye aliteuliwa kuwa kiongozi wa familia ya Odinga baada ya kifo cha babake, alisema anaendelea kumheshimu Dkt Oburu kama mzee wa familia, mlezi na kiongozi wa kisiasa. Alisema humshauri mara kwa mara kuhusu masuala ya kifamilia na pia ya kisiasa. "Tulizungumza kuhusu masuala ya familia na hafla ya kukabidhi serikali eneo la kujenga kaburi la heshima la Baba. Bila shaka tulijadili pia siasa na maisha kwa ujumla, lakini kwa sasa tunazingatia suala lililo mbele yetu," alisema Raila Junior. Aidha, Raila Junior alimweleza Dkt Oburu kuhusu azma yake ya kuwania ubunge wa Embakasi South katika uchaguzi wa 2027. Wiki juzi akiwa Homa Bay, Bw Raila Jnr aliwaomba wakazi wa Nyanza kumuunga mkono kisiasa, akisema ana uwezo wa kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi. Kama dada yake Winnie Odinga, ambaye ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Raila Junior pia analenga kuingia katika siasa za uchaguzi, ishara kwamba familia ya Odinga itaendelea kuwa sehemu ya siasa ambazo baba yao aliitawala kwa miongo kadhaa. Bi Winnie pia ametangaza nia ya kuwania wadhifa wa kisiasa nchini na anatarajiwa kugombea ubunge katika Kaunti ya Nairobi. Hata hivyo, bado hajafanya uamuzi wa mwisho iwapo atawania kiti cha Kibra au Lang'ata, maeneo yanayotambuliwa kuwa ngome ya kisiasa ya marehemu Raila.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.