WIRE โ MGAWANYIKO wa kisiasa umeibuka ndani ya kambi ya Rais William Ruto baada ya Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki, kupinga hadharani wito wa Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, wa kutaka Mlima Kenya Mashariki utengane kisiasa na wenzao wa Mlima Kenya Magharibi. Mvutano huo unajiri siku chache baada ya ushindi wa upinzani katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou kufufua mjadala kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya, ambalo lina idadi ya juu ya wapigakura. Akizungumza katika ibada ya shukrani ya Dayosisi ya Anglikana ya Embu katika Chuo cha Ualimu cha St Mark's Kigari, Kaunti ya Embu, Profesa Kindiki alisema hataruhusu juhudi zozote za kuligawa eneo hilo kisiasa. "Sitaki watu wetu waanze kuzungumza lugha tofauti. Tumefanya mambo mengi pamoja, tuna historia ndefu na hakuna kinachoweza kuleta mgawanyiko. Kama Naibu Rais nitahakikisha Mlima Kenya unabaki umeungana. Kwa sasa mimi ndiye Naibu Rais na nitahakikisha jamii zetu zinaendelea kutembea pamoja," akasema. Aidha, aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kuendelea kumuunga mkono Rais Ruto, akisema hiyo ndiyo njia bora ya kuhakikisha eneo hilo linatoa rais 2032. "Nataka tuwe na mazungumzo ya kweli na watu wetu. Baada ya William Ruto, ni sisi. Ile timu nyingine tuko nambari 20; tutafikiwa baada ya miaka 200," akasema. Kauli ya Profesa Kindiki inaenda kinyume na matamshi ya awali ya Bw Ruku ambaye amekuwa akirindima ngoma ya Mlima Kenya Mashariki kuwa na msimamo wake wa kisiasa na kiuchumi. "Ninapozungumzia mgawanyiko, ninarejelea masuala ya siasa za eneo letu. Nikiona jambo haliko sawa nitalizungumzia." Naibu Rais yuko sahihi kuhusu kuwaunganisha Wakenya," akasema Bw Ruku akikanusha ametofautiana na rais. Baadaye akiwa katika Kanisa la AIC Kabartonjo, Baringo Kaskazini, Bw Ruku alisema Mlima Kenya Mashariki umeamua kubaki ndani ya Kenya Kwanza na hautashawishiwa na kampeni za kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua. Pia alipuuza madai kwamba ushindi wa upinzani katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou unaashiria Rais Ruto amepoteza uungwaji mkono wa Mlima Kenya. ย "Gachagua anajigamba baada ya ushindi wa Ol Kalou akidai anadhibiti kura za Mlima Kenya. Kama Raila alikaribia kushinda bila kuungwa mkono na Mlima Kenya, Gachagua anategemea vipi kumshinda Rais Ruto 2027?" akauliza. Kwa mujibu wa mdadisi wa kisisa Prof Gitile Naituli mjadala wa kugawa Mlima Kenya unasukumwa zaidi na maslahi ya kisiasa kuliko maendeleo. "Mtu anayepaswa kuwa na wasiwasi ni Prof Kindiki. Hatakiwi kuruhusu mjadala wa mgawanyiko iwapo ana matumaini ya kumrithi bosi wake mnamo 2032. Hakuna atakayekuchukulia kwa uzito katika siasa za kitaifa ikiwa hujaunganisha ngome yako," akasema
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.