WIRE โ€” AKILI Mnemba (AI) inazidi kujitokeza kama teknolojia itakayobadilisha sekta ya kilimo barani Afrika huku Soko la Pamoja la Eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) likiendesha juhudi za kuunganisha sera za kidijitali ili kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji, kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kupata huduma za nyanjani kwa urahisi. Akizungumza jijini Nairobi wakati wa mafunzo ya uhamasishaji kuhusu matumizi ya AI na teknolojia zinazoibuka, Afisa wa Mawasiliano wa Sekretarieti ya COMESA, Leonard Chitunda, alisema AI tayari inaleta mageuzi katika kilimo kupitia utoaji wa taarifa muhimu kwa wakati ufaao. Afisa huyo alisema teknolojia hiyo inasaidia wakulima kupata utabiri wa hali ya hewa, taarifa za afya ya udongo, pembejeo zinazofaa, pamoja na mwenendo wa masoko ili kufanya maamuzi bora. "AI ni teknolojia inayogusa sekta nyingi. Inaongeza uzalishaji wa kilimo, inaboresha ufuatiliaji wa tabianchi na kuongeza ufanisi katika huduma mbalimbali," alisema Chitunda. COMESA inatekeleza mpango wa Inclusive Digitalisation for Eastern and Southern Africa unaofadhiliwa na Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola 2.5 bilioni (Ksh323.7 bilioni). Kati ya fedha hizo, Dola 10 milioni (Ksh1.3 bilioni) zimetengwa kwa COMESA kuandaa sera za pamoja, viwango na kujenga uwezo wa AI na mageuzi ya kidijitali. [caption id="attachment_190224" align="aligncenter" width="300"] Afisa wa Mawasiliano wa Sekretarieti ya COMESA, Leonard Chitunda. Picha|Sammy Waweru[/caption] Kiwango kikubwa cha fedha hizo kitaelekezwa kwa nchi wanachama kuboresha miundombinu ya kidijitali na huduma za intaneti ili wakulima, hasa wa maeneo ya vijijini, waweze kupata huduma za kilimo mtandaoni. Chitunda alisema AI inasaidia kuziba pengo lililosababishwa na upungufu wa maafisa wa nyanjani kwa kuwawezesha wakulima kupata ushauri wa kitaalamu kupitia simu na majukwaa ya kidijitali. "Wakulima wanaweza kupata ushauri kuhusu mbegu bora, matumizi ya pembejeo, hali ya hewa na mifugo inayofaa kwa maeneo yao bila kumwona afisa wa nyanjani ana kwa ana," alisema. Aliongeza kuwa COMESA inaendesha utafiti wa kikanda kubaini maeneo yatakayofaidika zaidi na AI, matokeo ambayo yatatumika kuandaa mkakati wa pamoja wa matumizi ya teknolojia hiyo. Mkurugenzi wa ICT katika Idara ya Serikali ya Biashara nchini Kenya, Timothy Were, alisema AI tayari inatumika katika sekta mbalimbali ikiwemo benki, afya, usafirishaji na sasa kilimo. [caption id="attachment_190223" align="aligncenter" width="300"] Mkurugenzi wa ICT katika Idara ya Serikali ya Biashara nchini Kenya, Timothy Were. Picha|Sammy Waweru[/caption] "AI inasaidia wakulima kupata taarifa za masoko, utabiri wa hali ya hewa, tahadhari za milipuko ya wadudu na magonjwa, pamoja na ushauri wa kitaalamu unaowasaidia kupunguza hasara na kuongeza uzalishaji," alielezea. Hata hivyo, Were alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sheria na sera zinazofanana katika nchi za COMESA ili kuhakikisha usalama wa mifumo ya kidijitali na kuzuia uhalifu wa mtandaoni. Wadau wanaamini kuwa utekelezaji wa mkakati wa AI wa COMESA utaifanya teknolojia hiyo kuwa nguzo muhimu ya mageuzi katika kilimo, kwa kuboresha upatikanaji wa taarifa, kuimarisha huduma za nyanjani na kusaidia wakulima kuhimili changamoto za tabianchi huku wakifikia masoko kwa urahisi zaidi.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.