WIRE โ€” AFISA Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Wakulima Kenya (KENAFF), Dkt Daniel Mwenda M'Mailutha, amechaguliwa kuwa Rais wa Shirika la Wakulima Duniani (WFO), hatua inayoiweka Kenya katika dira ya ulimwengu kwenye majadiliano ya kimataifa kuhusu kilimo, biashara ya mazao ya shambani, mabadiliko ya tabianchi na ustawi wa wakulima. Dkt Mwenda alipata ushindi huo baada ya uchaguzi wenye ushindani mkali uliofanyika wakati wa mkutano wa WFO Nairobi kati ya Juni 8 na 10, 2026. Alimshinda Fiona Simpson wa Australia kwa kura saba pekee kati ya kura 81 zilizopigwa, na hivyo kuwa Mkenya wa kwanza na Mwafrika wa pili kuongoza shirika hilo la kimataifa. "Haikuwa kazi rahisi. Ulikuwa ushindani mkali sana," aliambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee. Ushindi wake umepongezwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe na aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Fedha Nduati Kariuki, aliyesema uchaguzi huo umeipa Kenya hadhi katika sekta ya kilimo duniani. [caption id="attachment_190227" align="aligncenter" width="300"] Mkenya, Dkt Daniel Mwenda M'Mailutha, ambaye amechaguliwa kuwa Rais wa Shirika la Wakulima Duniani (WFO) pia ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Wakulima Kenya (KENAFF). Picha|Sammy Waweru[/caption] "Hii ni mara ya kwanza kwa mwanachama kutoka nchi inayoendelea kukua, hasa barani Afrika, kuchaguliwa kuongoza shirika hili tangu WFO irithi Shirikisho la Kimataifa la Wazalishaji wa Kilimo (IFAP). Kuchaguliwa kwa Mkenya kuongoza shirika hili la kimataifa ni uthibitisho wa weledi na uongozi ambao Kenya imeendelea kuonyesha katika jukwaa la kimataifa. Isitoshe, inaonyesha kuwa sifa na uwezo ndiyo vigezo pekee vya uteuzi, Kenya ina vipaji vya kiwango cha kimataifa vinavyostahili kuboreshwa," alisema Bw Kariuki, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ndani ya KENAFF. Dkt Mwenda alisema nafasi hiyo si mafanikio yake binafsi pekee, bali pia fursa kuhakikisha sauti ya wakulima inasikika katika taasisi za kimataifa zinazounda sera za kilimo, ikiwemo FAO, IFAD, WFP, Umoja wa Mataifa (UN) na majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi. Kwa miaka miwili ijayo atawakilisha wakulima kutoka Afrika, Asia, Ulaya, Amerika Kaskazini, Amerika Kusini na Oceania. Ajenda yake imejengwa kwenye nguzo tatu. Ya kwanza ni kuimarisha umoja wa WFO ili wakulima duniani wazungumze kwa sauti moja kuhusu uzalishaji wa chakula, biashara na sera za tabianchi. "Nguzo ya pili ni kukuza matumizi ya teknolojia ya kidijitali na upatikanaji wa huduma za kifedha. Kupitia mpango wa Sauti ya Mkulima, KENAFF imekuwa ikiunda wasifu wa kidijitali wa wakulima unaoonyesha historia yao ya uzalishaji, jambo linalorahisisha kupata mikopo kutoka benki na vyama vya ushirika. Hilo ni muhimu kulipandisha ngazi katika WFO," Dkt Mwenda akaelezea. [caption id="attachment_190226" align="aligncenter" width="300"] Dkt Daniel Mwenda M'Mailutha, aliyechaguliwa kuwa kuongoza Shirika la Wakulima Duniani (WFO) akielezea kuhusu sera zake wakati wa mahojiano jijini Nairobi mnamo Julai 9, 2026. Picha|Sammy Waweru[/caption] Alisema mfumo huo unaweza kusaidia mamilioni ya wakulima wadogo barani Afrika na maeneo mengine kupata fedha kwa urahisi na kwa gharama nafuu. Aidha, Dkt Mwenda anatarajia kutumia nafasi yake kushinikiza serikali za Afrika kutekeleza ahadi za Maputo (2003), Malabo (2014) na Kampala (2025) zinazotaka angalau asilimia 10 ya bajeti za kitaifa kuelekezwa kwenye sekta ya kilimo. Nguzo ya tatu, kulingana na Rais huyo mpya wa WFO inalenga kuboresha mifumo ya ufugaji. Alisema mifugo ni chanzo muhimu cha chakula, kipato na utamaduni katika jamii nyingi, hivyo mjadala wa kimataifa unapaswa kuangazia namna ya kufanya ufugaji uwe endelevu badala ya kuutazama kama chanzo pekee cha uzalishaji wa gesi chafu. "Kenya imeandikisha mafanikio makubwa katika sekta ya maziwa yanayoweza kuigwa duniani, yakichangiwa na ushirika imara, ushiriki wa wanawake na vijana pamoja na huduma bora za ugani." Dkt Mwenda anatarajia kuzindua mpango wake rasmi wa uongozi mwezi Agosti mwaka huu, 2026, akisema lengo lake kuu ni kuhakikisha wakulima wanasalia kitovu cha maamuzi ya kimataifa kuhusu mustakabali wa kilimo na usalama wa chakula.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.