WIRE — SERIKALI jana ililazimika kuzima tovuti rasmi ya Rais William Ruto baada ya wadukuzi kuivamia na kuweka ujumbe wa vitisho pamoja na kudai walipwe Bitcoin tano, za thamani ya takriban Sh41.3 milioni. Wakenya waliojaribu kufungua tovuti ya president.go.ke Jumamosi walikuta maudhui ya kawaida yameondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na ujumbe uliomlenga Rais Ruto. Wadukuzi hao walidai kuwa watafichua taarifa ambazo hawakuzitaja iwapo hawangelipwa fedha hizo. "Huu ni ujumbe wa tatu kwako kabla hatujafichua kila kitu kukuhusu. Lipa Bitcoin tano kwenye pochi hii ya Bitcoin ikiwa unataka amani kabla ya saa kumi na mbili jioni," ulisema ujumbe huo. Pia waliweka anwani ya pochi ya Bitcoin na kutaja majina ya watu watatu. Muda mfupi baadaye, tovuti hiyo ilizimwa na kuwekwa ujumbe unaosema ilikuwa ikifanyiwa matengenezo. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali, William Kabogo, alithibitisha shambulio hilo na kusema Mamlaka ya ICT ilianzisha mara moja utaratibu wa kukabiliana na tukio hilo. "Baada ya kugundua shambulio hilo, Mamlaka ya ICT ilianzisha taratibu zilizowekwa za kushughulikia matukio ya usalama wa mtandao," alisema Kabogo. Alisema tovuti hiyo ilisitishwa kwa muda ili kuruhusu uchunguzi wa kitaalamu, kudhibiti athari za shambulio na kurejesha huduma. Kabogo alisema hatua za kukabiliana na tatizo hilo tayari zilichukuliwa na kazi ya kurejesha tovuti  kuendelea. Aliongeza kuwa hadi sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa wadukuzi waliiba taarifa muhimu au kufikia data muhimu za serikali. "Hakuna ushahidi wa mtu asiyeidhinishwa kufikia taarifa muhimu, kuiba data au kupotea kwa taarifa. Mifumo ya serikali na huduma za kidijitali zinaendelea kufanya kazi kwa usalama," alisema. Aliongeza kuwa Mamlaka ya ICT inashirikiana na mashirika mengine ya serikali pamoja na wataalamu wa teknolojia kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha shambulio hilo. Iwapo serikali ingelipa kiasi kilichodaiwa, ingetoa karibu Sh41.3 milioni, kwa kuwa Bitcoin moja kwa sasa ina thamani ya takriban Sh8.27 milioni. Kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hii, Mkuu wa Huduma ya Mawasiliano ya Rais Munyori Buku na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed hawakuwa wamejibu simu wala ujumbe wa kutaka maoni yao kuhusu tukio hilo. Hili ni shambulio la pili kubwa dhidi ya mifumo ya serikali katika kipindi cha miezi michache. Mnamo Novemba 2025, wadukuzi walivuruga tovuti ya Rais pamoja na zile za Wizara za Usalama wa Ndani, Afya, Elimu, Kazi na Nishati. Pia walilenga Idara ya Uhamiaji, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Hazina ya Hasla na Serikali ya Kaunti ya Nairobi. Baada ya mashambulizi hayo, Wizara ya Usalama wa Ndani ilisema yalitekelezwa na kundi lililojitambulisha kama PCP@Kenya. Mwaka 2023, mfumo wa eCitizen pia uliangushwa na wadukuzi, hali iliyokatiza zaidi ya huduma 5,000 za serikali kabla ya kurejeshwa. Serikali ilisema wakati huo kuwa hakuna taarifa za wananchi zilizovuja. Shambulio hili linajiri huku Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu akiendelea kuonya kuhusu udhaifu wa mifumo ya ICT katika taasisi za umma. Katika ripoti zake za ukaguzi, Gathungu amesema taasisi nyingi za serikali hazina sera madhubuti za ICT, zina udhibiti hafifu wa mifumo, hazina mipango ya kuendelea kutoa huduma wakati wa dharura na zina mapungufu katika usimamizi wa mifumo ya kidijitali. Alionya kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha shughuli za serikali na usalama wa taarifa muhimu za umma. Miongoni mwa mifumo iliyotajwa kuwa na mapungufu ni eCitizen, ambayo ilibainika kukosa sera iliyoidhinishwa ya ICT, mpango wa kuendelea na shughuli wakati wa dharura, kamati ya ICT na kituo mbadala cha kuhifadhi taarifa. Aidha, Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA) imekuwa ikionya kuwa uelewa mdogo wa wafanyakazi kuhusu mashambulizi ya mtandaoni, pamoja na kuongezeka kwa mashambulizi yanayotumia Akili Unde (AI), kumeongeza hatari ya taasisi za umma kuvamiwa na wadukuzi.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.