WIRE โ SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna amesema chama cha ODM kimepoteza mwelekeo wake wa kisiasa na sasa maamuzi yake yanafanywa kutoka Ikulu. Akizungumza jana akiwa na Gavana wa Siaya, James Orengo baada ya mkutano wa waratibu wa mrengo wa Linda Mwananchi kutoka kaunti 36, Sifuna alisema chama hicho kimepoteza uhuru wake wala hakifanyi tena maamuzi kutoka makao yake ya Orange House. "Kwa bahati mbaya, maamuzi yanayoathiri ODM na wanachama wake hayafanywi tena Orange House. Hata uamuzi wa kuniondoa kama Naibu Kiranja wa Wachache ulitoka Ikulu. Inasikitisha kuona yaliyokumba chama chetu," alisema. Kauli hiyo inajiri siku chache baada ya Sifuna kuondolewa pia katika wadhifa wa Naibu Kiranja wa Wachache katika Seneti. Wakati huo huo, alitangaza kuwa mrengo wa Linda Mwananchi utaanza mikutano ya kisiasa nchini kote kuanzia Jumamosi katika Kaunti ya Taita Taveta, ikiwa sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Alisema kampeni hiyo inalenga kuimarisha miundo ya mrengo huo kuanzia ngazi ya kaunti hadi mashinani, huku ukitetea masuala yanayowahusu wananchi wa kawaida. "Mkutano wa Taita Taveta ndio mwanzo wa safari ya kuzunguka nchi nzima kuimarisha miundo yetu na kusikiliza matatizo ya Wakenya," alisema. Sifuna alisema viongozi waliokutana ni wanaharakati wa muda mrefu waliomsaidia kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa miaka mingi, lakini sasa wameamua kuendeleza azma hiyo kupitia mrengo wa Linda Mwananchi. "Hawa ndio askari wa mashinani. Tumefanya kazi pamoja kwa muda mrefu kutimiza ndoto ambayo Baba Raila Odinga alikuwa akiipigania. Tunawapongeza kwa kukataa kushawishiwa na madaraka na mali na kuamua kuendelea kutetea maslahi ya Wakenya," alisema. Aidha, aliikosoa serikali ya Rais William Ruto kwa sera zake za uchumi, akisema ushuru mkubwa umeathiri uwezo wa wananchi kununua bidhaa na kufanya biashara nyingi kuyumba. "Taarifa tulizonazo zinaonyesha biashara nyingi zinadorora kwa sababu uwezo wa Wakenya wa kununua bidhaa umeshuka kutokana na sera za serikali, hasa ongezeko la ushuru," alisema. Alisisitiza kuwa Linda Mwananchi itaendelea kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kushinikiza utawala unaowajali wananchi na kuendelea kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza. Sifuna pia alikipongeza Chama cha Democratic Change Party (DCP) kwa kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou. Alisema ushindi huo umeonyesha kuwa wapigakura wanaweza kushinda vitisho, rushwa na ushawishi wa kisiasa. "Wakazi wa Ol Kalou wamethibitisha kuwa haijalishi serikali inatumia mbinu gani, iwe ni zawadi, vitisho au vurugu, uamuzi wa mwisho hubaki mikononi mwa wapigakura," alisema. Hata hivyo, alitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ichunguze madai ya utoaji rushwa kwa wapigakura na matumizi mabaya ya rasilimali za serikali wakati wa uchaguzi huo. "Tunataka uwajibikaji. Wale wote waliotumia rasilimali za serikali na kuwahonga wapigakura wachukuliwe hatua. Hatutaki hali kama hiyo ijirudie mwaka 2027 au katika uchaguzi mwingine wowote," alisema. Gavana Orengo alisema waratibu kutoka maeneo ambayo hapo awali yalikuwa ngome za ODM wamekubali kupanua shughuli za Linda Mwananchi kote nchini. "Tumeshuhudia ukuaji mkubwa wa vuguvugu hili. Kwa idadi ya watu tunaowaona wakiiunga mkono, Linda Mwananchi ndiyo vuguvugu la kisiasa linalokua kwa kasi zaidi nchini. Tumejitolea kulieneza katika kila kona ya Kenya," alisema.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.