WIRE โ VIONGOZI wa eneo la Pwani wakiongozwa na Mawaziri Hassan Joho (Madini), Salim Mvurya (Michezo na Vijana) pamoja na Spika wa Seneti Amason Kingi, wameanza mikakati ya kusaka kura milioni nne kutoka eneo hilo kumuunga mkono Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao. Viongozi hao, kwa ushirikiano na magavana wanaounga mkono serikali akiwemo Abdulswamad Nassir (Mombasa), Fatuma Achani (Kwale), Gideon Mung'aro (Kilifi), Andrew Mwadime (Taita Taveta) na Issa Timamy (Lamu), wameanza mikutano ya hadhara kuwahamasisha wakazi kujitokeza kujisajili kama wapiga kura na kuhakikisha wanapata vitambulisho vya kitaifa. Mikakati hiyo pia inahusisha maseneta wa eneo hilo pamoja na wabunge wengi wanaounga mkono serikali. Hata hivyo baadhi ya viongozi wa upinzani akiwemo Mbunge wa Wundanyi Danson Mwashako na mwenzake wa Nyali Mohammed Ali hawaungi mkono mpango huo. Viongozi hao wamekuwa wakiwahamasisha wananchi kumuunga mkono Rais Ruto, wakisema serikali yake imeanzisha miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wakazi wa Pwani licha ya eneo hilo kutompa kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. "Rais Ruto hakupata kura nyingi eneo la Pwani lakini alitukumbuka na kutuletea miradi ya maendeleo. Alirejesha shughuli na biashara katika Bandari ya Mombasa ambazo zilikuwa zimehamishwa hadi Naivasha na Nairobi. Pia alimteua Bw Joho katika Baraza la Mawaziri baada ya kushirikiana na aliyekuwa kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, na amewateua makatibu wakuu sita kutoka Pwani, ametufaa," alisema Bw Mvurya. Alisema viongozi wa pwani wameandaa ratiba ya kutembelea maeneo bunge yote ya Pwani ili kuwaeleza wananchi kuhusu miradi iliyotekelezwa na serikali ya Rais Ruto Wakisaka ungwaji mkono. "Tumepanga ratiba ya kwenda kila eneo bunge kueleza viongozi wa mashinani kuhusu serikali ya Rais. Tayari tumetembelea maeneo bunge ya Likoni, Matuga, Kaloleni na Jomvu, na sasa tuko Mvita kueleza umuhimu wa kumuunga mkono Rais Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2027. Tunafanya hamasa ili watu wetu wasihadaiwe na wale walioko upinzani," alisema. Alisema siasa za sasa zimejaa fitina, uhasama na umbea, akisema viongozi wa Pwani wanapaswa kuangazia changamoto zinazowakabili wananchi kama umaskini, ukosefu wa ajira na maendeleo. "Vita yetu hapa Pwani ni kupambana na umaskini, ukosefu wa ajira kwa vijana wetu na kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi. Hatutaingia katika vita vya kisiasa vya wengine. Wale wanaompinga Rais hawajafanya chochote lakini wana maneno matamu ya kuambia watu ONETAM," alisema. Naye Seneta wa Mombasa, Mohammed Faki, aliwataka wakazi wa Pwani kujitokeza kwa wingi kuchukua vitambulisho na kujiandikisha kama wapiga kura ili kutumia nguvu yao ya kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao. Bw Faki alisema eneo la Pwani lina uwezo wa kutoa karibu kura milioni nne, lakini idadi hiyo haiwezi kufikiwa iwapo wananchi hawatashiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi. "Eneo la Pwani lina uwezo wa kutoa karibu kura milioni nne ambazo tunaweza kuziweka kwenye debe. Lakini changamoto ni kwamba si watu wote wanaopiga kura. Tuna tatizo kubwa la watu kutokuchukua vitambulisho. Kila kijana mwenye umri wa miaka 18 na zaidi aende akachukue kitambulisho," alisema. Alisema kama vile Mombasa ilivyoongoza katika usajili wa bima ya afya ya SHA, wanataka eneo hilo pia liwe mstari wa mbele katika usajili wa wapiga kura. Bw Faki na Gavana Nassir walisema uchaguzi mkuu ujao utakuwa fursa kwa wakazi wa Pwani kuonyesha shukrani kwa serikali ya Rais Ruto kwa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika eneo hilo. Walitaja hatua kama vile utoaji wa boti za kisasa kwa wavuvi, kushughulikia changamoto za ardhi, ujenzi wa masoko, barabara na miradi mingine ya miundombinu kama baadhi ya mafanikio ya serikali hiyo. Gavana Nassir alisema Pwani haipaswi kupinga uwekezaji unaoletwa katika eneo hilo, bali viongozi wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata sehemu yao katika maendeleo ya kitaifa. "Kwa miaka mingi tumekuwa tukishuhudia miradi ya maendeleo katika maeneo mengine ya nchi. Jukumu letu ni kuwaelekeza wananchi kwa ukweli na kuhakikisha eneo hili linasalia kwenye meza ya kitaifa ya kisiasa," alisema.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.