WIRE โ MWAKA 1979, waanzilishi wa Brown's Food Company waliamua kujaribu bahati yao katika sekta ya maziwa wakianza na ng'ombe wawili pekee.ย Zaidi ya miongo minne baadaye, jaribio hilo limekua na kuwa kampuni inayotambulika kwa utengenezaji wa jibini (cheese) nchini Kenya na katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Awali kampuni hiyo iliyojulikana kama Brown's Cheese, ilianzishwa na David na Sue Brown kama biashara ya kutengeneza vifaa vya kuongeza joto kwenye nyumba (solar heaters) vinavyotumia nishati ya jua, huku wakifuga ng'ombe wachache kwa ajili ya maziwa ya matumizi ya familia. Kulingana na Delia Andrew, Mkurugenzi Mkuu mwenza wa kampuni hiyo, kilichoanza kama jaribio dogo la kutafuta suala la maziwa kwenye familia, sasa kimegeuka kuwa biashara kubwa ya mseto wa bidhaa za maziwa. Leo hii kampuni hiyo huzalisha majibini yanayoweza kuuzwa kwa zaidi ya Sh100,000 moja, huku ikilenga soko la bidhaa za thamani ya juu ndani na nje ya Afrika Mashariki. "Wazazi wetu walipoanzisha biashara walikuwa wakitengeneza hita (vifaa vya joto) za sola huku wakifuga ng'ombe wachache wa maziwa ya nyumbani. Kulipotokea ukame wa muda mrefu, jibini aina ya cheddar lilipungua sokoni, ndipo wakaamua kujaribu kulitengeneza nyumbani," anasema Delia, ambaye anamiliki kampuni hiyo pamoja na mumewe. Anasema jaribio hilo liligeuka kuwa somo lao la kwanza la ujasiriamali, kwamba fursa nyingi huzaliwa wakati wa changamoto. Kilichoanza kama shughuli ya familia kilianza kuvutia marafiki na wateja waliotaka kununua majibini zaidi, na hatimaye uzalishaji kibiashara ukabisha hodi. Tangu mwanzo, familia hiyo ilifuata falsafa ya kutengeneza bidhaa ambazo wao wenyewe wangekuwa tayari kuzitumia kabla ya kuzipeleka sokoni. Delia anasema msimamo huo umeisaidia kampuni kudumisha viwango vya juu vya ubora hata ilipoendelea kukua. Alipojiunga na biashara hiyo karibu miaka 16 iliyopita, alikuta ikiwa bado imejikita zaidi katika uzalishaji wa shambani lakini ikiwa na ndoto ya kupanuka. Anaeleza kuwa hapo ndipo walipoanza kujenga mifumo rasmi ya usimamizi, udhibiti ubora na kuongeza aina mbalimbali za bidhaa. "Mchango wetu uliifanya kampuni iimarike, ambapo mifumo, ubora na utofauti wa bidhaa vilikuwa msingi wa maendeleo," alisema katika mahojiano na 'Akilimali Dijitali'. Mojawapo ya maamuzi ya kwanza chini ya uongozi wake ilikuwa kufungua milango ya shamba kwa wageni na wateja. Anaamini hatua hiyo ilijenga uwazi na kuimarisha imani ya walaji bidhaa wanazounda. "Walaji leo hawataki kununua tu bidhaa. Wanataka kujua zinakozalishwa na kwa namna gani," alisema. [caption id="attachment_190142" align="aligncenter" width="300"] Majibini yaliyoundwa mwaka huu na Brown's Food Company, Limuru, Kaunti ya Kiambu. Picha|Sammy Waweru[/caption] Kadri miaka ilivyopita, Brown's Food Company ilipanua shughuli zake zaidi ya utengenezaji wa jibini na kuingia katika usagaji wa unga. Delia anasema waligundua kuwa biashara haiwezi kutegemea bidhaa moja pekee. "Hatukuegemea maziwa pekee. Tulilazimika kutathmini mfumo mzima wa kilimo kuanzia afya ya udongo, mazao, mifugo hadi lishe," anaelezea. Kwa sasa kampuni hiyo huchakata zaidi ya lita 20,000 za maziwa kila siku kutoka kwa takriban wakulima 6,000 katika maeneo ya Molo, Kinangop na Embu. Aidha, maziwa hayo huzalisha bidhaa mbalimbali, ingawa jibini ndiyo bidhaa yenye thamani kubwa zaidi na inayohitaji utaalamu wa hali ya juu. Delia anasema kampuni imekuwa ikipanuka hatua kwa hatua kulingana na uwezo wake na mahitaji ya soko. Ingawa mtaji wa upanuzi zaidi bado ni changamoto, wameamua kuepuka kukopa kupita kiasi. "Nidhamu hiyo ndiyo imetuwezesha kusalia imara," anasema. Leo hii Brown's Food Company imeajiri wafanyakazi 300, kutoka wafanyakazi 25 pekee alipotwaa uongozi miaka 16 iliyopita. Karibu asilimia 25 ya uzalishaji wake husafirishwa kwenda Tanzania, Uganda na Rwanda, huku ikipanga kuingia masoko ya Dubai na China. Delia anasisitiza kuwa kutengeneza jibini si shughuli ya kawaida ya viwandani bali ni mchakato wa kibayolojia. "Jibini ni bidhaa hai. Huboreka na kukomaa kadri muda unavyosonga," alisema wakati wa mahojiano. Baadhi ya majibini hukomaa baada ya miezi kadhaa, huku mengine yakihifadhiwa kwa miaka sita ili kuongeza ladha na thamani yake. Gurudumu la jibini lenye uzani wa kilo 25 linaweza kuuzwa kwa zaidi ya Sh100,000, huku kilo moja ya jibini lililokomazwa kwa miaka sita ikiuzwa kwa angalau Sh4,000. Tofauti na maziwa, jibini huongezeka thamani kadri linavyozeeka, jambo lililoifanya kampuni hiyo kuwekeza katika vyumba maalum vya kukomaza jibini vinavyodhibiti joto na unyevunyevu. Brown's Food Company huzalisha aina mbalimbali za majibini yakiwemo mozzarella, pizza cheese, parmesan, gouda, camembert, brie na feta. Hali kadhalika, hutengeneza maziwa mala, maziwa gururu (yoghurt), siagi na aiskrimu, baadhi zikiungwa kwa matunda yanayonunuliwa kutoka kwa wakulima. [caption id="attachment_190143" align="aligncenter" width="300"] Majibini ya saizi na uzito tofauti yaliyoundwa na Brown's Food Company. Picha|Sammy Waweru[/caption] Licha ya mafanikio hayo, kampuni hiyo inakabiliwa na changamoto za usambazaji, hasa kudumisha mifumo baridi kutoka kiwandani hadi sokoni. "Ukivunja mfumo wa kudhibiti hali ya joto, ubora wa bidhaa hauwezi kurejeshwa. Ndiyo maana tuliwekeza katika magari yetu wenyewe ya usambazaji yenye mifumo ya baridi," anasema. Changamoto nyingine ni kuhakikisha ubora wa maziwa unabaki wa kiwango kinachotakiwa, hasa kwa majibini yanayohifadhiwa kwa muda mrefu. Phineas David, anayesimamia udhibiti wa ubora, anasema Brown's Food Company imeanzisha vituo vya kukusanya na kupoza maziwa Embu, Molo na Kinangop ili kuhakikisha ubora unaanzia shambani. Anasema kampuni sasa hupokea hadi lita 35,000 za maziwa kwa siku. Wakulima hupata huduma za mifugo, mafunzo na pembejeo, huku wakilipwa mara mbili kwa mwezi kupitia akaunti zao za benki. "Ubora huanzia shambani. Maziwa yakiharibikia huko, hakuna kiwango cha usindikaji kitakachoyarejesha," anasema. Hata hivyo, kupanda kwa bei ya maziwa, gharama za uzalishaji na ushuru kumeongeza shinikizo kwa kampuni. Hali hiyo imeifanya kuendelea kubuni njia mpya za kuongeza mapato. Kupitia nembo ya Groven Meadow, kampuni hiyo imeingia katika usagaji wa unga wa nafaka asili kama vile mtama, wimbi na aina mbalimbali za maharagwe ili kuhamasisha lishe bora na kuhifadhi bayoanuwai. Aidha, Delia anasema Brown's Food Company imeanza kutathmini uwezekano wa kutengeneza majibini ya mimea kutokana na ongezeko la watu wasioweza kutumia bidhaa zenye lactose. "Kuna watumiaji wasiovumilia lactose, hivyo tunatafuta njia mbadala โ kujumuisha mimea bila kuacha misingi yetu ya ubora na uadilifu," anadokeza.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.