WIRE — MAMLAKA ya Kitaifa ya Usalama wa Viumbehai (NBA) imezitaka taasisi zinazofanya utafiti wa viumbe vilivyobadilishwa na kuboreshwa vinasaba (GMO) kuzingatia kikamilifu hatua za usalama wakati wa majaribio ya shambani yaliyodhibitiwa ili kulinda afya ya binadamu, mifugo na mazingira. Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa NBA, Dkt Ann Karimi, alisema watafiti wanapaswa kufuata masharti ya Sheria ya Usalama wa Viumbehai ya mwaka 2009 huku Kenya ikiendelea kuendeleza utafiti wa bayoteknolojia unaolenga kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza uzalishaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. [caption id="attachment_190131" align="aligncenter" width="300"] Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa NBA, Dkt Ann Karimi wakati wa mahojiano Kalro, Kandara, Murang'a. Picha|ammy Waweru[/caption] Akizungumza wakati wa ziara ya ujumbe wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Viumbehai ya Senegal katika vituo vya Shirika la Utafiti wa Masuala ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo (Kalro) vya Muguga na Kandara, kaunti ya Kiambu na Murang'a mtawalia, alisema ni muhimu taasisi za kilimo kuzingatia sheria za majaribio. NBA, na taasisi za serikali kama vile Kalro inaendelea na majaribio ya mimea kadha iliyoboreshwa vinasaba ikiwemo mihogo, mahindi na viazimbatata. "Majaribio yanaendelea vizuri na tutaendelea kushirikiana na Kalro kuhakikisha Kenya inadumisha viwango vya juu vya usalama katika maendeleo na udhibiti wa GMO," Dkt Karimi alisema. [caption id="attachment_190132" align="aligncenter" width="300"] Muhogo ulioboreshwa vinasaba uliovunwa kutoka shamba la Kalro, Kandara, Murang'a. Picha|Sammy Waweru[/caption] Katika vituo vya Muguga na Kandara, watafiti wanaendeleza utafiti na majaribio ya viazi vinavyostahimili ugonjwa wa late blight pamoja na mihogo inayojihimili dhidi Cassava Brown Streak Disease na Cassava Mosaic Disease, magonjwa ambayo yamekuwa yakipunguza uzalishaji barani Afrika. Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Bayoteknolojia ya KALRO, Dkt Martin Mwirigi, alisema utafiti huo unalenga kuzalisha mazao yanayostahimili athari za tabianchi, wadudu na magonjwa huku yakilinda afya ya umma na mazingira. "Pamba ya Bt imekuwa ikilimwa nchini tangu mwaka 2020 baada ya kuidhinishwa kwa kilimo cha kibiashara, bila kuripotiwa madhara kupitia mifumo ya ufuatiliaji ya NBA," alibainisha afisa huyo. [caption id="attachment_190133" align="aligncenter" width="300"] Dkt Ann Karimi (katikati), Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Viumbehai (NBA), akitoa maelezo kwa ujumbe kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Viumbehai na Wizara ya Kilimo ya Senegal kuhusu muhogo ulioboreshwa kwa teknolojia ya vinasaba (GM Cassava) katika kituo cha KALRO Kandara, Murang'a. Muhogo huo, unaosubiri kuidhinishwa kwa matumizi ya kibiashara, unalenga kukabiliana na magonjwa ya Cassava Brown Streak Disease (CBSD) na Cassava Mosaic Disease (CMD). Picha|Sammy Waweru[/caption] Mazao yanayofanyiwa utafiti na majaribio nchini ni pamoja na mahindi ya Bt, mahindi yanayostahimili ukame, viazi vitamu na mihogo inayostahimili virusi, pamoja na viazi vya GMO. Kenya, hata hivyo, kesi zilizowasilishwa kortini kuzuia usambazaji wa bidhaa za GMO zinatatiza azma ya ukumbatiaji wa bayoteknolojia. Mwaka 2022, baada ya Rais William Ruto kutwaa uongozi aliondoa marufuku ya miaka 10 ya GMO – hatua ambayo ilifungua jamvi la kesi za kuipinga kortini. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usalama wa Viumbehai nchini Senegal, Prof Aliou Ndiaye, alisema nchi yake imejifunza mengi kutokana na uzoefu wa Kenya katika utafiti na udhibiti wa GMO, maarifa ambayo yataisaidia kuimarisha mfumo wake wa usalama wa viumbehai.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.