WIRE โ€” KIZAAZAA kilizuka katika mahakama kuu ya Milimani Jumanne mwanaharakati Julius Kamau alipovua shati akabaki nusu uchi baada ya Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kudai wanaume watatu waliokamatwa Kiamaiko eneo la Mathare mnamo Juni 19, 2026 hawako mikononi mwa polisi. Baada ya wakili Paul Nyamondi anayemwakilisha IG Kanja kusema hayo, Jaji Alexander Muteti aliwaamuru mkuu huyu wa polisi na mkurugenzi wa uchunguzi wa jinai Mohamed Amin kufika kortini Julai 20, 2026 (Jumatatu ijayo) kueleza kule waliko - Michael Oloo, Evans Otieno na MacMillan Mugo. Hata kabla ya Bw Nyamondi kukamilisha sentensi hiyo kuhusu hatma ya wahasiriwa, Bw Kamau alifyatuka mahala alipokuwa ameketi akatoa shati huku akipiga duru akisema "Kenya imeisha. Tumenyanyaswa vya kutosha sasa, tunauawa, tunaibiwa, tumeteswa vya kutosha. Kama nikufa nife leo." Akiwa nusu uchi, alisongea karibu na Jaji Alexander Muteti akilalama vikali huku wazazi na jamaa wa wahanga hao pamoja na wanaharakati waliozidi 15 wakijifunika bendera ya Kenya wakipasua vilio na kila mmoja kuongea lugha yake. Walivuruga shughuli mahakamani kwa kupiga duru wooooi.. huku wakilia na kupiga mayowe na kelele za kila aina wakisema "serikali inateka nyara na kuua watoto wasio na hatia." Mama na jamaa za wahasiriwa - Michael Oloo, Evans Otieno na MacMillan Mugo - walipasua vilio huku wakidondokwa na machozi wakisema "sasa ni siku 26 na hatujui watoto wako wapi." Wakaendelea: "Ni aibu kwa Inspekta Jenerali Douglas Kanja kusema hajui watoto wetu wako wapi na ndiye kinara wa usalama wetu sote." Kina mama wengine yamkini jamaa wa karibu wa wahasiriwa walianguka na kugaagaa sakafuni wakilia wakiuliza "kweli tutatoa watoto wengine wapi. Hata mtu akizaa atalea saa gapi na uchumi ndio huu umezorota, hatuna pesa na nchi inaenda segemnege." Baba wa mmoja wahasiriwa hao alisimama na kuchomoka nje mbio akipiga duru na kurudi tena kortini akisema "Kenya imegauka kuwa Haiti. Sasa tuko Haiti. Rais William Ruto anasukuma nchi hii kutumbukia pabaya. Hatuna tofauti na Haiti sisi Kenya." Huku akitetemeka, baba huyo alisaidiwa na polisi alipoanguka na kuzirai. Hali kortini iligeuka ikawa ni kama mnara wa Babeli kila mmoja akiongea lugha yake huku mawakili Abner Mango, Ian Mutiso na John Ndegwa wakishindwa kuwatuliza wanaharakati na wazazi wa wahasiriwa. Wakati huu wote Jaji Alexander Muteti aliendelea kuandika uamuzi huku hali ikitokota. Mwanaharakati Julius Kamau aliyevua shati alikamatwa na kupelekwa seli huku wenzake wakichacha kwa kupiga duru. Ilikuwa hali ya mshike mshike. Mawakili wa wahasiriwa waliomba mahakama iamuru IG na DCI wafike kortini wenyewe kueleza waliko wahasiriwa. Jaji Muteti aliombwa aamuru IG na DCI wawasilishe majibu katika muda wa siku tatu kueleza walikowapeleka wanaume hao watatu. Bw Mutiso alieleza korti kwamba aliyekuwa rubani Mwenda Mbijiwe alitoweka hivyo yapata miaka minne sasa na polisi walidai hawakumshika. Mbijiwe bado hajulikani aliko. "Naomba hii mahakama iamuru IG na DCI wafike kortini kueleza waliko wateja wetu," Bw Mutiso alimrai Jaji Muteti. Akitoa uamuzi, Jaji Muteti aliwaamuru Kanja na Amin wafike kortini kueleza waliko wahasiriwa. "Suala hili la kutoweka kwa watu halieleweki kabisa. Ikiwa polisi hawajui kule waliko wahasiriwa nani atajua," Jaji Muteti alimuuliza wakili wa serikali. Oloo alikamatwa Juni 19, 2026 alipoenda kinyozi. "Oloo alichukuliwa kutoka kwa kinyozi na hajulikani alipelekwa wapi alipokamatwa na kuingizwa ndani ya Subaru," Jaji Muteti alifahamishwa. Jaji huyo hatimaye alizishauri familia za wahasiriwa ziwe na subira korti iwachukulie hatua wahusika. Kesi iliahirishwa hadi Julai 20, 2026 kwa maagizo zaidi.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.