WIRE โ MFUNGWA wa zamani ameshangaza wengi baada ya kumtafuta hakimu aliyemhukumu kifungo cha miaka minne gerezani ili kumshukuru. Kila siku ya kazi saa tatu kamili asubuhi, Hakimu Mkazi Eugene Pascal Nabwana huketi katika Mahakama Nambari Moja ya Wamunyu, Kaunti ya Machakos, kusikiliza kesi mbalimbali, lakini asubuhi ya Julai 2 ilikuwa tofauti. Karibu dakika 10 pekee kabla ya aanze shughuli zake za kila siku, msimamizi wa mahakama pamoja na msaidizi wa mahakama walimfuata na kumwomba akutane kwa muda mfupi na mtu aliyekuwa akimsubiri nje. Mwanzoni hakimu huyo alisita, lakini baada ya kushawishiwa alikubali. Alipotoka nje alimkuta mwanaume aliyeonekana mwenye wasiwasi. Muda mfupi baadaye, mgeni huyo alimshukuru kwa kifungo cha miaka minne alichotumikia gerezani, akisema ndicho kilichogeuza maisha yake na kumtia hamasa ya kutafuta elimu. Miaka minne iliyopita, akiwa Hakimu Mkazi katika Mahakama ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu, takribani kilomita 620 kutoka Wamunyu anapohudumu sasa, Bw Nabwana alikuwa amemhukumu Mwendwa Kilatya Nthenge, 35, kifungo cha miaka minne jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa mifugo. Baadaye, Bw Nabwana alihamishwa na kuwa Mkuu wa Kituo katika Mahakama ya Wamunyu, nafasi anayoshikilia hadi sasa. Bw Kilatya alitumikia kifungo chake katika Gereza la Hindi GK, Kaunti ya Lamu, kati ya mwaka 2023 na 2026. Aliposimama tena mbele ya hakimu huyo, mfungwa huyo wa zamani alieleza kuwa alipokuwa gerezani alijiunga na Mpango wa Elimu Magerezani na kujiandikisha kufanya mtihani wa KCSE na kupata wastani wa alama ya D (Plain). "Nina furaha kukutana nawe tena, mheshimiwa. Ulinifunga miaka minne gerezani. Sijaja kulipiza kisasi bali kukushukuru sana. Baada ya kunihukumu, ulifika Gereza la Hindi na kutuhimiza wafungwa, akiwemo mimi, kwamba bado tunaweza kusoma tukiwa gerezani. Nilichukua ushauri wako kwa uzito," alisema Bw Kilatya. Baada ya kutoka gerezani, Bw Kilatya alisema amekuwa akifanya vibarua mbalimbali ili kujikimu na kuweka akiba kidogo, lakini hana uwezo wa kifedha wa kujiunga na chuo kikuu. Kwa sababu hiyo, alimwomba hakimu huyo amshauri, amwelekeze au amsaidie kupata ufadhili ama watu wanaoweza kumwezesha kutimiza ndoto yake ya kuendelea na masomo. "Ndoto yangu ni kujiunga na chuo kikuu nianze kwa kusomea cheti cha Usimamizi na Utawala wa Biashara. Kutoka hapo nitaendelea kupanda ngazi za elimu hatua kwa hatua. Changamoto ni kwamba sina Sh240,000 zinazohitajika kukamilisha kozi hiyo. Natamani kujiunga na Chuo Kikuu cha Africa Nazarene ambako kozi hiyo inatolewa. Naomba msaada," alisema Bw Kilatya. Bw Nabwana aliahidi kuwashirikisha wadau mbalimbali na wasamaria wema ili kumsaidia kufanikisha ndoto yake. Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Nabwana alisema kukutana tena na Bw Kilatya kulikuwa ushahidi kwamba wakati mwingine adhabu ya mahakama inaweza kuwa mwanzo wa mageuzi makubwa ya maisha ya mtu. "Sikuwahi kufikiria jambo kama hilo lingeweza kutokea," alisema Bw Nabwana. Hakimu huyo alisema kilichomgusa zaidi ni kwamba Bw Kilatya hakumwomba fedha za chakula wala msaada wa kutafutiwa kazi. "Nimeanza kuwatafuta watu mbalimbali ili tuone kama tunaweza kumpatia fedha hizo. Nilimpongeza kwa kupata alama ya D akiwa gerezani, huku akifundishwa na walimu watatu wa kujitolea. Hilo pekee ni mafanikio makubwa. Kinachonifurahisha zaidi ni kwamba bado ana hamu kubwa ya kuendelea na masomo yake," alisema Bw Nabwana. Alisema simulizi ya Bw Kilatya ni mfano mmoja tu wa mabadiliko mengi yanayotokea ndani ya mfumo wa mahakama lakini mara nyingi hayapati nafasi ya kusimuliwa. Kwa mujibu wa Bw Nabwana, maafisa wa mahakama hushuhudia watu wengi wakibadilika na kuwa bora zaidi baada ya kupitia mkondo wa sheria.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.