WIRE โ€” KAMPENI za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou zilipokamilika rasmi Jumatatu, wapigakura walibaki wakitafakari masuala matatu tofauti yaliyotawala kampeni kabla ya uchaguzi wa Alhamisi. Swali kuu lililozua mjadala ni iwapo uchaguzi huo unafaa kuwa kura ya maoni kuhusu utawala wa Rais William Ruto, kama kinavyosisitiza chama cha Democracy for Citizens Party (DCP). Suala jingine ni iwapo wakazi wanapaswa kukiunga mkono chama tawala UDA ili kuendeleza miradi ya maendeleo na kuonyesha kuwa Nyandarua inaweza kuamua hatima yake ya kisiasa bila kushawishiwa na kaunti jirani za Mlima Kenya. Hoja ya tatu ni kwamba wapigakura wapuuze siasa za kitaifa na wamchague mgombeaji wanayeamini ndiye anayefaa zaidi kuwakilisha Ol Kalou. Tofauti na chaguzi zilizopita, mikutano ya kampeni haikutoa taswira halisi ya uungwaji mkono wa kisiasa. Mikutano ya UDA na DCP ilihudhuriwa na makundi yaliyokuwa yakizunguka kutoka mkutano mmoja hadi mwingine bila kujali chama kilichoandaa. Wadadisi wa kisiasa wanakadiria kuwa zaidi ya nusu ya waliohudhuria mikutano mikubwa walikuwa sehemu ya makundi hayo. Isitoshe, tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo wafuasi walivaa mavazi ya vyama vyao kipindi chote cha kampeni, wengi walikuwa wakivua kofia na fulana mara tu mikutano ilipomalizika. Haikuwa jambo la kushangaza kuona mtu mmoja akiwa na kofia za UDA na DCP na kuzivaa kulingana na mkutano aliokuwa akihudhuria. Katika kampeni zote, viongozi wa DCP walieleza kuwa uchaguzi huo ni nafasi ya kumwaadhibu Rais Ruto na serikali yake kufuatia kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kile walichodai ni usaliti dhidi ya eneo la Mlima Kenya. Wakiongozwa na Seneta wa Nyandarua John Methu, viongozi hao walidai kuwa miradi mingi ya maendeleo iliyozinduliwa wakati wa kampeni ilikuwa mbinu ya kuwahonga wapigakura. Ujumbe huo ulitawala pia mkutano wa mwisho wa DCP uliofanyika katika Bustani ya Ol Kalou Jumatatu. "Ni lazima tukatae mgombeaji wa UDA kwa sababu Rais Ruto alitusaliti baada ya kumpa uungwaji mkono mkubwa katika uchaguzi mkuu wa 2022. Kumkataa yeye na mgombeaji wake kutarejesha heshima ya kisiasa ya jamii yetu. Kenya nzima inaangalia Nyandarua kwa sababu uchaguzi huu utaweka msingi wa kumwondoa mamlakani 2027," akasema Seneta Methu. Mgombeaji wa DCP Kamau Ngotho aliwataka wapigakura kutumia uchaguzi huo kuonyesha kutoridhishwa kwao na serikali ya Kenya Kwanza. "Kura ya DCP ni ujumbe mzito kwa Kenya na dunia dhidi ya mauaji ya waandamanaji wa Gen Z, gharama ya juu ya maisha na mfumo wa afya unaodorora," akasema. Kwa upande wake, UDA iliwataka wapigakura kutenganisha siasa za kitaifa na maendeleo ya eneo lao. Chama hicho kilisema Nyandarua imekuwa ikitengwa kwa miaka mingi na kwamba kuunga mkono serikali kutahakikisha miradi inayoendelea inakamilika. Mratibu wa kampeni za UDA na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nyandarua Faith Gitau aliwashutumu viongozi wa DCP kwa kutumia malalamishi ya eneo hilo kisiasa ilhali walipokuwa serikalini hawakutekeleza maendeleo. "Wanaozungumzia usaliti walikuwa katika nyadhifa za juu serikalini lakini hawakufanyia Nyandarua maendeleo. Aliyekuwa Naibu Rais atuambie ni mradi gani mkubwa aliouletea kaunti hii. Miradi mingi mnayoiona sasa ilianzishwa baada ya kuondoka kwake," akasema katika mkutano wa mwisho wa UDA katika uwanja wa JM Kariuki KMTC.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.