WIRE โ WAKATI mamia ya wageni wa humu nchini na kutoka mataifa mbalimbali walipofurika katika Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara ya Maua (IFTEX) jijini Nairobi, kampuni moja ya Kenya ilivutia wengi kwa ubunifu wa kipekee uliosimamisha shughuli katika Ukumbi wa Visa Oshwal. Banda la Ole Engai Growers lilikuwa miongoni mwa yaliyopigwa picha zaidi katika maonyesho hayo ya mwaka huu, 2026 baada ya kuwasilisha sanamu ya farasi mwenye ukubwa wa wastani wa mnyama huyo, iliyotengenezwa kwa maua mabichi yaliyolimwa kwenye mashamba ya kampuni hiyo. Farasi huyo wa maua, aliyebuniwa kuadhimisha Mwaka wa Farasi katika kalenda ya Mwaka Mpya wa Kichina, aliunganisha sanaa na kilimo kwa njia iliyovutia wageni katika maonyesho yaliyofanyika kati ya Juni 2 na 4. Sanamu hiyo ilionekana kana kwamba ilikuwa hai kutokana na umbo lake lililoundwa kwa ustadi mkubwa, likiwa na kichwa, manyoya shingoni, mwili na miguu iliyopambwa kwa maua meupe, ya kijani na ya krimu. Ua aina ya gypsophila ndilo lililotumika zaidi kuunda mwili wa farasi huyo, likimpa mwonekano mweupe na laini kama wingu. Muundo huo uliashiria nguvu, kasi na ustahimilivuโsifa zinazohusishwa na farasi katika utamaduni wa Kichina, na pia ukuaji wa kampuni hiyo katika sekta ya maua. "Mwaka huu, 2026, ni Mwaka wa Farasi kulingana na kalenda ya Kichina. Tulitaka kuonyesha nguvu, ukuaji na uvumilivu kama kampuni kupitia maua tunayozalisha wenyewe," alisema Mkurugenzi Mwenza kampuni hiyo, Anjili Shah. Anjili alieleza kuwa wazo hilo lilibuniwa na timu ya kiufundi ya kampuni ikiongozwa na mbunifu mkuu ambaye amekuwa akiandaa mabanda yaliyoshinda tuzo katika maonyesho ya IFTEX kwa miaka kadhaa. Ubunifu huo uliiwezesha Ole Engai Growers kutwaa Tuzo ya Fedha ya Ubora wa Ubunifu (Silver Award for Design Excellence), baada ya mwaka uliopita kushinda tuzo ya banda bora zaidi. [caption id="attachment_190053" align="aligncenter" width="300"] Tuzo ya Ole Engai Growers baada ya kutumia muundo wa farasi wenye mvuto wakati wa Maonyesho ya IFTEX 2026. Picha|Sammy Waweru[/caption] Mwanzilishi mwenza na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Sanir Shah, alisema maonyesho hayo yalionyesha uwezo wa kampuni hiyo kuzalisha maua ya kiwango cha juu na kubuni kazi za kipekee bila kutegemea maua kutoka kwa wazalishaji wengine. "Ole Engai Growers huzalisha maua katika shamba lenye ukubwa wa karibu hekta 29 eneo la Kaptagat, Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu," Sanir alifichua. Mbali na gypsophila, kampuni hiyo pia hulima maua aina ya delphinium ya rangi mbalimbali, asters, kangaroo paws, dianthus na kiwi mellow kulingana na mahitaji ya soko. Kulingana na Sanir, kampuni hiyo huuza nje takribani tani 1,200 za maua kila mwaka, masoko makubwa yakiwa Ulaya huku Mashariki ya Kati ikiandikisha ukuaji wa oda. Hata hivyo, alisema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji wa mizigo kwa njia ya ndege. "Miaka mitano iliyopita tulikuwa tukilipa karibu Dola 1.4 za Amerika kwa kilo moja ya maua kusafirishwa. Sasa gharama imevuka Dola 4 kwa kilo. Hii imeathiri faida yetu," alisema. Baraza la Maua Kenya (KFC), pia, limeeleza kuwa gharama hizo zimeongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, jambo linaloongeza gharama za usafirishaji wa bidhaa zinazoharibika haraka kama maua. [caption id="attachment_190054" align="aligncenter" width="300"] Ole Engai Growers huzalisha maua katika shamba lenye ukubwa wa karibu hekta 29 eneo la Kaptagat, Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu. Picha|Sammy Waweru[/caption] "Kwa sasa, usafirishaji pekee unachangia zaidi ya asilimia 40 ya gharama zote za kuuza maua nje wakati wa msimu wa mauzo bora," anasema Clement Tulezi, Afisa Mkuu Mtendaji KFC. Aidha, bei ya mbolea imeongezeka kwa karibu asilimia 25 huku gharama za uzalishaji zikiongezeka kwa kati ya asilimia 20 na 30. Changamoto nyingine ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yamevuruga ratiba za uzalishaji kutokana na mvua zisizotabirika. Anjili alisema hali hiyo imefanya upangaji wa shughuli za shambani kuwa mgumu zaidi. Licha ya changamoto hizo, Ole Engai Growers inaendelea kupanua uzalishaji na kutafuta masoko mapya, hasa Mashariki ya Kati ya nchi za Uarabuni. Kwa ujumla, sekta ya maua nchini Kenya inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi. Mwaka 2025 iliiingizia nchi karibu Dola milioni 845 za Amerika (zaidi ya Sh110 bilioni), huku Kenya ikiendelea kuuza maua katika zaidi ya nchi 60 duniani, asilimia 70 ya mauzo hayo yakielekezwa katika soko la Umoja wa Ulaya (EU).
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.