WIRE โ€” HUKU upinzani ukiendelea kuonyesha wana umoja hadharani, mvutano mkali unaendelea kushuhudiwa kati ya mrengo wa Linda Mwananchi na Umoja wa Upinzani, kila upande ukipambana kudhibiti kampeni za kumng'oa madarakani Rais William Ruto. Migawanyiko hiyo ilijitokeza wazi Ijumaa baada ya aliyekuwa Naibu Rais ,Rigathi Gachagua, kumshambulia Gavana wa Murang'a, Irungu Kang'ata, kuhusu uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. "Nimesikia Kang'ata akisema anataka kuja Ol Kalou akiwa na Linda Mwananchi. Hatukuhitaji hapa. Kama unataka kupigia debe UDA, Jubilee au chama kingine chochote, uko huru kufanya hivyo, lakini kampeni za DCP ni suala la wenyeji," akasema Bw Gachagua. Kauli hiyo iliwafanya viongozi wa Linda Mwananchi kuhamisha mikutano yao Nyahururu na kusitisha mipango ya kumpigia kampeni mgombea wa DCP. Bw Kang'ata alijiunga na Linda Mwananchi mwezi uliopita wakati wa mkutano wa kisiasa uliofanyika Thika. Matamshi ya Bw Gachagua dhidi ya Bw Kang'ata yamefichua mapambano makubwa zaidi ya kupigania ushawishi ndani ya upinzani. Duru kutoka upinzani zinaeleza kuwa baadhi ya viongozi wana hofu kwamba ajenda yao ya kisiasa inaweza kudhoofishwa na kundi la Linda Mwananchi ilhali wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali tangu 2022. Magharibi mwa Kenya Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, amemkosoa Bw Sifuna akisema hana ushawishi wowote wa kisiasa. "Nataka kusema Sifuna hana kura Kakamega na Bungoma Didmus Barasa amemshinda kwa umaarufu. Eugene Wamalwa ndiye mwanasiasa maarufu zaidi ambaye ataleta kura kwa upinzani bila kujali atashikilia wadhifa gani," akasema Bw Salasya. "Wamejaa kiburi na wanataka kuleta mkanganyiko. Wania urais tuone utakakofika na jinsi itakavyomalizika," akaongeza Bw Salasya. Si mara ya kwanza kwa mbunge huyo kupuuza ushawishi wa kisiasa wa Bw Sifuna na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya katika eneo hilo. Mrengo wa Sifuna na Natembeya umeitikisa kambi ya DAP-Kenya. Wawili hao sasa wanapanga mikutano miwili mikubwa ya kisiasa katika kaunti za Trans Nzoia na Bungoma Julai 25 na 26. Bw Natembeya tayari ametangaza kuwa atatetea kiti chake kupitia chama kipya cha kisiasa badala ya DAP-Kenya kinachoongozwa na Bw Wamalwa. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, Bw Natembeya na Bw Wamalwa walitofautiana kuhusu uongozi wa DAP-Kenya, hali iliyomfanya gavana huyo kuanzisha vuguvu la Tawe. Wakati wa ziara ya upinzani Magharibi mwa Kenya mwezi uliopita, Bw Gachagua alimtangaza Bw Natembeya kuwa mratibu wa kampeni zake Magharibi. Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, naye amewashutumu baadhi ya wanasiasa kwa kujaribu kuelekeza shughuli za Linda Mwananchi huku wakimtumia Bw Sifuna kuendeleza maslahi yao binafsi. Alimtaja Bw Kang'ata kuwa mmoja wa viongozi wanaochochea migawanyiko ndani ya upinzani. "Linda Mwananchi haitatekwa nyara nikiwa macho. Hatutakuruhusu wewe (Kang'ata) kumtumia vibaya mwana wetu Edwin Sifuna," akasema Bw Amisi, ambaye amekuwa akiongoza kampeni za chama chake cha People Renaissance Movement (PRM) katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Seneta wa Kisii, Richard Onyonka ,anaamini kuwa hatimaye makundi hayo mawili yataungana chini ya muungano mmoja, akisema migawanyiko ya sasa inadhoofisha upinzani. Bw Onyoka amesisitiza kuwa pande zote mbili zinapaswa kuweka kando kiburi na kushirikiana. "Lazima tushirikiane kwa sababu ajenda ya Upinzani na Linda Mwananchi ni kuhakikisha utawala wa sasa unaondolewa madarakani mwaka ujao," akasema Bw Onyonka, ambaye yuko ndani ya Linda Mwananchi lakini anaunga mkono azma ya urais ya Dkt Matiang'i.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.