WIRE โ MBUNGE wa Nyaribari Chache, Zaheer Jhanda, Jumamosi alijitokeza hadharini wiki moja baada ya kuhusishwa na uvamizi dhidi ya msafara wa Linda Mwananchi eneo la Keumbu, Kaunti ya Kisii. Bw Jhanda jana alisema hakuna mtu ambaye atamtishia licha ya kuamrishwa afike mbele ya Idara ya Upelelezi Nchini (DCI). Uvamizi dhidi ya kambi ya Linda Mwananchi ulisababisha mauti ya mtu mmoja na kuwajeruhi wengine. Jumamosi, mbunge huyo alihutubia mamia ya wafuasi wake katika eneo la Keumbu. Alikuwa ameamrishwa afike mbele ya DCI kutokana na tukio hilo la Julai 3 ambapo kando na maafa ya mtu mmoja, wengine 20 walijeruhiwa. "Hapa inaitwa nini?" akauliza ambapo umati ulijibu "Keumbu" Umati aliouhutubia ulijumuisha vijana na akina mama huku akiongea kwa lugha ya Ekegusii. "Nchi lazima ijue kuwa kuna mbunge wa Nyaribari Chache ambaye yupo Keumbu, nyumbani na haogopi" Kujitokeza kwake kunajiri wakati ambapo kuna uchunguzi unaoendelea kutokana na uvamizi wa msafara wa Linda Mwananchi ambao uliongozwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna. Aliyekuwa Jaji Mkuu, David Maraga, ambaye alikuwa kwenye msafara wa Linda Mwananchi alinusurika bila kujeruhiwa ingawa gari lake liliharibiwa vibaya. Vincent Osiemo maarufu kama Mapinduzi aliaga dunia baada ya kupigwa na mawe na kuanguka kwenye mojawapo ya magari kisha akapigwa na umati. Upasuaji wa maiti ambao ulifanywa na Mwanapatholojia wa serikali, Dkt Peter Morebu, ulibaini kuwa marehemu aliaga dunia kutokana na majeraha ya kichwa ambayo yalisababishwa na kupigwa kwa kifaa butu. Maandalizi ya mazishi yamekuwa yakiendelea nyumbani kwao Gionseri, eneobunge la Bobasi huku akitarajia kuzikwa mnamo Julai 17. Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) imetangaza kuwa imewanyaka washukiwa saba kuhusiana na ghasia hizo za Keumbu. Hata hivyo, washukiwa hao waliachiliwa huru baada ya kufikishwa kortini bila afisa wa uchunguzi au kiongozi wa mashtaka. Ingawa hivyo, polisi nao wanasisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na wote waliohusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.