WIRE โ€” BAADA ya takriban miaka saba ya kusubiri haki, Mahakama Kuu jijini Nairobi Ijumaa ilihitimisha moja ya kesi zilizotikisa taifa kwa kumpata aliyekuwa Meja wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Peter Mugure Mwaura, na hatia ya kumuua mkewe Joyce Syombua pamoja na watoto wao wawili. Jaji Martin Muya alisema upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka yoyote kwamba Mugure alipanga mauaji hayo kwa umakini, akayatekeleza ndani ya Kambi ya Jeshi la Anga ya Nanyuki, kisha akashirikiana na mtu mwingine kuficha miili ya marehemu kwa kuizika eneo la Thigithu, Kaunti ya Laikipia. Kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Joyce, mwenye umri wa miaka 31, alisafiri kutoka Nairobi hadi Nanyuki Oktoba 25, 2019 akiwa na watoto wake Shanice Maua, 10, na Prince Michael, 5, baada ya Mugure kuwaalika kwa kile kilichoonekana kuwa mkutano wa kifamilia. Siku iliyofuata walionekana wakiondoka kambini pamoja kabla ya kula chakula cha mchana katika Hoteli ya Kilimara Springs. Huo ndio ulikuwa mwisho wao kuonekana wakiwa hai. Jaji Muya alisema baada ya kurejea kambini, Mugure aliwaua watatu hao, akaweka miili yao kwenye mifuko maalumu ya kuhifadhia maiti na kuificha kwenye buti la gari lake kabla ya kwenda kuizika kwa siri Thigithu. Mahakama ilisema mauaji hayo hayakuwa ya ghafla. Ushahidi ulionyesha kuwa siku tatu kabla ya tukio, Mugure alikuwa ametembelea eneo hilo akiwa na afisa mwingine, hatua ambayo ilimshawishi jaji kuwa tayari alikuwa amechagua mahali pa kuficha miili kabla ya kutekeleza mpango wake. Shahidi muhimu katika kesi hiyo alikuwa Collins Pamba, aliyekiri kusaidia kuondoa miili. Alieleza kuwa alipofika nyumbani kwa Mugure alikuta mwili wa Joyce ukiwa ndani ya mfuko wa maiti huku miili ya watoto ikiwa kwenye bafu. Alisema walifunga miili kwa kamba, wakaiweka ndani ya buti la gari baada ya kuondoa tairi la akiba ili kupata nafasi zaidi, kisha wakaitoa kambini na kuizika. Ingawa alikiri kushiriki kuficha ushahidi, Pamba alifanya makubaliano na upande wa mashtaka, akakiri kosa dogo na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani. Jaji alisema ushahidi wake uliungwa mkono na ushahidi wa kisayansi. Uchunguzi wa DNA uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali ulithibitisha kuwa mabaki yaliyopatikana kaburini yalikuwa ya Joyce, Shanice na Prince Michael. Aidha, vipimo vilionyesha kwa uwezekano wa asilimia 99.9 kwamba Mugure alikuwa baba wa watoto hao wawili. Ripoti ya uchunguzi wa maiti ilionyesha Joyce alifariki kutokana na majeraha makubwa ya kupigwa, huku watoto wote wawili wakinyongwa. Mahakama pia ilibaini kuwa kulikuwa na sababu ya kifedha nyuma ya mauaji hayo. Joyce alikuwa amepata amri ya mahakama iliyomtaka Mugure kulipa Sh25,000 kila mwezi kama matunzo ya watoto, lakini alilipa mara moja pekee kabla ya kumshawishi asafiri hadi Nanyuki. Jaji Muya alitupilia mbali utetezi wa Mugure kwamba aliwaacha watoto kwa rafiki wa Joyce, akisema hakuna ushahidi uliounga mkono na kwamba familia hiyo haikuwahi kutoka kambini ikiwa hai. Kwa msingi huo, mahakama ilimpata Mugure na hatia katika mashtaka yote matatu ya mauaji, ikisema upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake bila shaka yoyote. Atahukumiwa Julai 14, 2026.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.