WIRE โ SERIKALI inaendelea kusukuma mpango wake wa kupanda miti bilioni 15 ifikapo 2032 kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kurejesha mazingira yaliyoharibiwa. Hata hivyo, wanaharakati wa mazingira wanaonya kuwa mafanikio ya mpango huo yanaweza kutatizwa na ongezeko la miradi ya maendeleo inayopendekezwa ndani ya misitu asili. Kwa mujibu wa wanamazingira, hali ya sasa inaibua kinaya. Wanasema huku serikali ikihamasisha wananchi kupanda mabilioni ya miche ya miti, sehemu nyingine za misitu inaendelea kukatwa ili kupisha ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege, nyumba za serikali na miradi mingine ya miundombinu. Rais William Ruto, ambaye kabla ya kuingia katika siasa alisomea Botania, Zoolojia na Ikolojia ya Mimea katika Chuo Kikuu cha Nairobi, amefanya uhifadhi wa mazingira kuwa mojawapo ya nguzo kuu za utawala wake. Serikali yake imeweka lengo la kupanda miti bilioni 15 ndani ya miaka kumi ili kuongeza kiwango cha misitu nchini na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, tangu alipoingia madarakani mwaka 2022, serikali imelaumiwa kwa kuruhusu miradi mbalimbali inayopangwa ndani ya misitu. Hali hiyo imezua maswali kuhusu iwapo juhudi za kurejesha mazingira zinaenda sambamba na kulinda misitu ya asili ambayo imekuwepo kwa miongo mingi. Takwimu za ripoti ya hali ya uchumi zinaonyesha kuwa eneo la mashamba ya miti ya serikali liliongezeka kutoka hekari 143,900 mwaka 2021 hadi hekari 148,600 mwaka 2025. Pia kasi ya upanzi wa miti iliongezeka baada ya kuzinduliwa kwa mpango wa kitaifa, huku maelfu ya hekari zikipandwa miche mipya kila mwaka. Lakini wakati huo huo, ukataji wa miti katika mashamba ya serikali ulirejelewa baada ya kuondolewa kwa marufuku ya miaka sita, ingawa baadaye mahakama ilisimamisha uamuzi huo. Kwa wanaharakati wa mazingira, changamoto kubwa si uvunaji wa miti pekee bali kutumiwa kwa misitu asili kwa miradi ya maendeleo. Wanasema kila barabara, njia ya umeme au jengo linalojengwa ndani ya msitu hupunguza uwezo wa mfumo wa ikolojia kuendelea kufanya kazi ipasavyo. Wasiwasi huo uliongezeka baada ya Bunge kupitisha Sheria ya Marekebisho ya Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu ya mwaka 2025, ambayo inaruhusu Huduma ya Misitu Kenya (KFS) kutoa nafasi kwa ujenzi wa barabara, njia za umeme na miundombinu mingine ndani ya misitu ya umma. Mojawapo ya miradi iliyozua mjadala mkubwa ni barabara ya Ihithe-Ndunyu Njeru inayopangwa kupita ndani ya Msitu wa Aberdare. Ripoti za tathmini ya mazingira zinaonyesha kuwa ujenzi huo utahitaji kukatwa kwa sehemu ya msitu wa mianzi, msitu wa milimani na maeneo ya nyasi. Wanaharakati wanaonya kuwa Aberdare ni mojawapo ya vyanzo muhimu vya maji nchini, ikihudumia mabwawa ya Sasumua na Ndakaini pamoja na kuchangia uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji. Kwa sababu hiyo, Mahakama ya Mazingira ilisimamisha mradi huo kwa muda huku kesi ikiendelea kusikilizwa. Katika Jiji la Nairobi, hofu kama hiyo imejitokeza kuhusu Msitu wa Ngong Road, ambapo sehemu ya ardhi imetengwa kwa miradi inayohusiana na Uwanja wa Talanta. Wanaharakati wanasema ujenzi wa barabara ya kuingia, eneo la wakandarasi na miundombinu mingine unaweza kuendelea kugawa msitu huo katika vipande vidogo. Kadhalika, katika Msitu wa Karura, ukataji wa baadhi ya miti mapema mwaka huu uliibua maswali kutoka kwa wanaharakati. Serikali ilieleza kuwa eneo hilo linatayarishwa kwa vitalu vya miche ya miti na makazi ya muda ya vijana wa Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS) wanaoshiriki katika mpango wa kupanda miti. Katibu wa Maendeleo ya Misitu, George Tarus, amesisitiza kuwa serikali haina mpango wa kuharibu misitu asili. Alisema tayari miti takriban1.9 bilioni imepandwa chini ya mpango wa kitaifa na kwamba miradi yote inayopendekezwa ndani ya misitu lazima ifanyiwe tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuidhinishwa. Kwa mujibu wake, lengo ni kurejesha mazingira yaliyoharibiwa katika misitu, maeneo ya malisho, mashamba na sehemu za kijani mijini, huku maendeleo muhimu yakiendelea kwa kuzingatia sheria za mazingira. Hata hivyo, wanaharakati wanasisitiza kuwa mafanikio ya mpango wa kupanda miti hayatapimwa kwa idadi ya miche iliyopandwa pekee. Wanasema kipimo kikubwa kitakuwa uwezo wa Kenya kulinda misitu yake ya kale na mifumo yake ya ikolojia dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na miradi ya maendeleo, ili juhudi za kurejesha mazingira zisiwe zinafutwa na uharibifu unaoendelea katika misitu asili.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.