WIRE โ BAADHI ya manifesto ambazo aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Amolo Odinga alitumia katika kampeni zake za urais zitakuwa sehemu ya masomo katika Chuo cha Uongozi na Utawala cha Raila Amolo Odinga kinachoanzishwa chini ya Chuo cha Serikali Kenya (KSG). Chuo hicho, kilichozinduliwa Jumanne na Rais William Ruto wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya KSG, kinalenga kuhifadhi na kufundisha falsafa za Raila kuhusu utawala bora, demokrasia, huduma kwa umma na maendeleo ya bara Afrika. Mkurugenzi Mkuu wa KSG, Profesa Nura Mohamed, alisema kundi la kwanza la wanafunzi linatarajiwa kuanza masomo mwezi Septemba. Alisema mtaala wa chuo hicho utajengwa juu ya nguzo tano kuu zilizotawala maisha ya kisiasa ya Raila; umoja wa Afrika, uongozi ushirikishi, utawala bora, elimu na ubunifu, pamoja na amani na haki. ย "Alipokuwa akiwania urais alikuwa na manifesto mbalimbali, na baadhi yake zitajumuishwa katika masomo ya chuo hiki ili maono yake yaweze kutekelezwa," alisema. Profesa Mohamed alisema walipolinganisha manifesto ya mwisho ya Raila na Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya Kenya Kwanza, waligundua kuwa zilikuwa na mambo mengi yanayofanana. Kwa mujibu wake, masomo katika chuo hicho yatakitwa kwa kuzingatia maono ambayo Raila alikuwa nayo kwa Kenya na bara la Afrika. Mbali na masomo, chuo hicho kitakuwa na maktaba itakayopewa jina la Raila Odinga pamoja na kituo cha kuhifadhi nyaraka, hotuba, maandishi na mchango wake katika uongozi na siasa. Aidha, kutakuwa na Kituo cha Ubunifu cha Chandaria kitakachofadhiliwa na mfanyabiashara Manu Chandaria, pamoja na Kituo cha Umahiri katika Huduma kwa Wateja na Uzalishaji kitakacholenga kuboresha utendaji wa watumishi wa umma. Profesa Mohamed alisema chuo hicho kinatarajia kuwaalika viongozi mashuhuri duniani kutoa mihadhara ya uongozi, akiwemo Rais wa zamani wa Amerika Barack Obama na marais wa sasa na wa zamani kutoka mataifa mbalimbali. Alisema lengo ni kufanya Kenya kuwa kitovu cha mijadala kuhusu mustakabali wa utawala bora, huduma kwa umma na maendeleo ya Afrika. Kwa mujibu wa kijitabu kinachoelezea malengo ya chuo hicho, taasisi hiyo itakuwa kitovu cha utafiti, ushauri wa sera na ubunifu wa suluhu kwa changamoto kama ufisadi, ukosefu wa ajira, umaskini, maendeleo ya miundombinu na ugatuzi. Pia itaanzisha vituo vya uchambuzi wa sera kwa wizara, Bunge, serikali za kaunti na Mahakama, kuchapisha ripoti za utabiri wa sera na kuandaa taarifa za kila robo mwaka kuhusu uzalishaji katika utumishi wa umma. Profesa Mohamed alisema chuo hicho kitawahudumia mawaziri, makatibu, viongozi waandamizi wa serikali na viongozi wachanga wanaojiandaa kuingia katika sekta ya umma na binafsi. Aliongeza kuwa madarasa ya viongozi wa ngazi za juu yatakuwa na washiriki kati ya 15 na 20 pekee ili kutoa nafasi ya mijadala ya kina kuhusu mikakati ya kubadilisha nchi za Afrika kupitia uongozi bora. Alisema pia chuo hicho kitatoa mpango wa malezi kwa viongozi vijana, ubunifu, afya ya akili kwa watumishi wa umma na kujenga hazina ya kidijitali ya maarifa kuhusu maisha na urithi wa Raila Odinga. "Urithi wa Raila utaendelea kuishi. Tumejizatiti kuhakikisha maono, ndoto na falsafa zake vinaendelea kuongoza juhudi za kuijenga Kenya na kuhamasisha Afrika," alisema Profesa Mohamed.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.