WIRE โ€” MATUMIZI ya dawa za kubadilisha rangi ya ngozi yaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya ikiwemo kuharibika kwa figo, mfumo wa fahamu, ngozi kuwa nyepesi na mabadiliko ya kudumu ya rangi ya ngozi, madaktari wameonya. Daktari mtaalamu wa ngozi katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Meru, Gacheri Kathiri, anasema bidhaa nyingi zinazotumiwa kubadilisha rangi ya ngozi huwa na kemikali hatari kama zebaki ambazo zinaweza kusababisha madhara yasiyoweza kurekebishwa kwa urahisi. Anasema baadhi ya watumiaji hupata chunusi kali, ngozi kupasuka, maambukizi ya mara kwa mara, shinikizo la damu, kisukari na hata matatizo ya figo kutokana na matumizi ya muda mrefu ya bidhaa hizo. Pia, anaonya kuwa matangazo mengi yanayodai ngozi nyepesi ndiyo ishara ya urembo huwa yanawapotosha hasa vijana na kuwafanya waanze kutumia bidhaa hizo bila ushauri wa kitaalamu. Onyo hilo linaakisiwa katika simulizi ya Anne Desdemona, 27, ambaye alitumbukia kwenye uraibu wa kubadilisha rangi ya ngozi akiamini ungeongeza mvuto wake. Kwa zaidi ya mwaka mmoja, alitumia zaidi ya Sh10,000 kila mwezi kununua krimu, sabuni na mafuta yaliyodaiwa kumfanya awe na ngozi nyepesi na laini. Hata hivyo, badala ya kuanza kujiamini, alianza kupata vipele vyenye maumivu, ngozi kupasuka kati ya vidole, upele mapajani na hofu ya watu kugundua alikuwa akibadilisha rangi ya ngozi yake. Alisema kila alipoacha kutumia bidhaa hizo kwa wiki chache, ngozi yake ilianza kurejea katika hali ya kawaida, jambo lililomfanya azidi kuzitumia. Safari yake ya kuacha uraibu huo ilianza baada ya kukutana na mpwa wake mwenye umri wa miaka 14 na akamuonya msichana huyo asitumie bidhaa hiyo kwa sababu ilikuwa hatari. Anasema mpwa wake alimuuliza swali lililomtikisa: "Kama ni mbaya, mbona wewe unaitumia?" Swali hilo lilimfungua macho. Kwa usaidizi wa daktari wa ngozi, Anne aliacha matumizi ya bidhaa hizo hatua kwa hatua na sasa anasema amejifunza kuwa uzuri wa kweli hauamuliwi na rangi ya ngozi bali afya ya ngozi na kujiamini.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.