WIRE โ WAFANYABIASHARA katika Soko la Keumbu, Kaunti ya Kisii, wanakabiliwa na wakati mgumu baada ya biashara yao kudorora kufuatia vurugu zilizotokea wakati wa mkutano wa kisiasa wa viongozi wa Linda Mwananchi Ijumaa iliyopita. Hali imezidi kuwa mbaya kutokana na kampeni kwenye mitandao ya kijamii inayowahimiza wananchi kususia bidhaa kutoka sokoni humo, kwa madai kwamba baadhi ya wafanyabiashara walihusika katika vurugu hizo. Ingawa hali ya usalama imeanza kutulia, wafanyabiashara wanasema idadi ya wateja imepungua kwa kiasi kikubwa na wengi wao sasa wanapata hasara. Bi Josephine Mang'ere alisema biashara ilikuwa ikiendelea vizuri kabla ya mkutano huo kuvurugika. "Tulikuwa tumewasubiri viongozi wa Linda Mwananchi, lakini baada ya muda mawe yakaanza kurushwa. Tangu siku hiyo biashara imekuwa ngumu. Tunapoenda kuuza bidhaa zetu watu hawazinunui. Tunaomba tusamehewe," alisema. Kwa upande wake, Bi Sophia Moraa alisema biashara yake ya parachichi imeathirika vibaya kwani wateja wengi wamekataa kununua mazao yake, hali iliyosababisha baadhi yake kuoza. "Sisi ni wafanyabiashara wasio na hatia. Tunapowafuata wateja barabarani wanatuambia tuuze bidhaa zetu kwa viongozi wanaotuhumiwa kusababisha vurugu. Tunataka siasa za amani," alisema. Bi Mary Moraa alisema wafanyabiashara sasa wanahimiza amani na kuheshimiana kisiasa. "Sisi ni wazazi. Kijana aliyefariki ni mtoto wetu pia, na kifo chake kinatuumiza. Wanasiasa wote waruhusiwe kuhutubia wananchi bila ubaguzi," alisema. Wakati huo huo, Meshack Yoge, mmoja wa manusura wa shambulizi dhidi ya msafara wa Linda Mwananchi, alisema anaamini alinusurika kifo kwa bahati. Bw Yoge, ambaye alijeruhiwa jicho baada ya kupigwa na jiwe, alisema tukio hilo lilikuwa la kutisha na bado hajapona kikamilifu. Alisema walikuwa wakielekea Keroka baada ya mkutano wa Kisii mjini na walipofika Keumbu, walivamiwa na kundi la watu waliokuwa wakirusha mawe na kubeba rungu, mishale na pinde. "Tuliona watu wakikimbia kuelekea kwetu wakipiga kelele wakisema, 'Waueni!' Dirisha la gari lilivunjwa, jiwe likanigonga usoni na kujeruhi jicho. Nilinusurika kupoteza jicho na meno," alisema. Aliongeza kuwa walilazimika kukimbia kwa kasi kuokoa maisha yao na baadaye akapelekwa hospitalini Keroka ambako alipatiwa matibabu. Mgombeaji wa udiwani wa Kisii Central, Bw Andrew Moindi Mochache, aliyekuwa ndani ya gari hilo, alisema waliona kifo wazi. "Niliona kifo kwa macho yangu. Watu waliotushambulia walikuwa wamekusudia kutuua," alisema. Kiongozi wa People's Liberation Party (PLP) Martha Karua na Mbunge wa North Mugirango Joash Nyamoko walilaani vurugu hizo, wakisisitiza kuwa siasa zinapaswa kuendeshwa kwa amani. Bi Karua alisema hakuna anayepaswa kuzuiwa kutoa maoni yake au kushiriki shughuli za kisiasa kwa amani, huku Bw Nyamoko akiwataka vijana kuepuka kutumiwa na wanasiasa kuchochea ghasia.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.