WIRE โ MICHELLE Wanjiru ana umri wa miaka 17, lakini tayari sauti yake inasikika katika mijadala ya kimataifa kuhusu usalama wa vijana mtandaoni. Ni mmoja wa wanachama wa Baraza la Vijana la TikTok, kundi linalowakutanisha vijana kutoka mataifa mbalimbali ili kuwashauri viongozi wa jukwaa hilo kuhusu changamoto zinazowakabili watumiaji vijana, ikiwemo matumizi ya Akili-Unde (AI), unyanyasaji mtandaoni, taarifa potofu na afya ya akili. Michelle anasema alijiunga na baraza hilo mwaka wa 2023 baada ya rafiki wa familia kumtumia tangazo la maombi. Hakutarajia kufanikiwa, lakini tangu wakati huo amegundua kuwa changamoto za mtandaoni haziwezi kutenganishwa na hali halisi ya maisha ya vijana. "Hakuna sera inayopaswa kutungwa kwa ajili yetu bila kwanza kutuuliza kuhusu changamoto tunazokumbana nazo. Keti nasi, tusikilize na utuelewe," anasema. Kulingana naye, watu wazima mara nyingi hutunga sera za kuwalinda vijana bila kuwashirikisha wale wanaoathiriwa moja kwa moja. Kupitia mpango wake uitwao Mind of a Queen, Michelle huandaa warsha kila likizo ya shule kwa wasichana kutoka Nairobi, Kiambu na Mombasa kujadili matumizi ya mitandao ya kijamii, urafiki na changamoto wanazokumbana nazo. Katika moja ya warsha hizo, msichana wa miaka 15 alimweleza kuwa alikuwa akifanya ngono na waendesha bodaboda ili apate fedha za kununua sodo, hali iliyomfanya apate ujauzito. Msichana mwingine wa miaka 13 alisema alidanganywa kuwa kufanya ngono kungepunguza maumivu ya hedhi kwa sababu hakuwahi kupewa elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi. "Hakuna mtoto anayestahili kupitia mateso kama hayo," anasema Michelle. Anaamini umaskini huwafanya wasichana kuwa katika hatari zaidi ya kulengwa mtandaoni. "Teknolojia haiondoi tofauti za kijamii. Mara nyingi huziongeza," anaeleza. Michelle anasema safari yake ya utetezi ilianza akiwa na miaka sita alipowaandikia viongozi wa serikali akitaka huduma bora za afya kwa watoto. Hatua hiyo ilimfundisha kuwa hata sauti ya mtoto inaweza kuwafikia viongozi. Baada ya shule kufungwa wakati wa janga la Covid-19, alianza kutumia TikTok. Anasema hakuwahi kuwa na ndoto ya kuwa mtayarishaji wa maudhui, bali alipenda kutazama video za burudani na kufuatilia mitindo mipya. "Wazazi wangu hawakunifuatilia kila dakika. Walinifundisha kuwajibika na kunihakikishia kuwa ningewaeleza kila nikikumbana na tatizo lolote mtandaoni," anasema. Anahimiza wazazi wajenge uhusiano wa kuaminiana na watoto wao badala ya kutegemea udhibiti pekee, akisema teknolojia hubadilika haraka kuliko uwezo wa mzazi kufuatilia kila hatari mpya. Katika Baraza la Vijana la TikTok, Michelle ameshiriki mijadala kuhusu ulinzi wa faragha, afya ya akili, taarifa potofu na matumizi ya AI. Anasema changamoto mpya huibuka kila mara. "Unatatua tatizo moja, jingine linaibuka," anasema. Kwa mujibu wake, AI imeongeza hatari ya video na picha bandia zinazoweza kuwapotosha au kuwaumiza vijana. Anasisitiza kuwa pamoja na kuweka alama kwenye maudhui yaliyotengenezwa kwa AI, vijana wanapaswa kufundishwa kuchambua taarifa wanazokutana nazo mtandaoni. Michelle anasema baadhi ya mapendekezo ya baraza hilo yamezaa matunda kupitia vipengele vipya vya TikTok vinavyowakumbusha watumiaji kupumzika baada ya kutumia muda mrefu, mazoezi ya kutuliza akili usiku na zana zinazowasaidia wazazi kusimamia matumizi ya watoto wao. Hata hivyo, anasema changamoto kubwa anayokutana nayo katika warsha zake ni hofu ya wasichana kuripoti au kuwazuia wanaowanyanyasa mtandaoni. "Hujiuliza, 'Nikimzuia atanifichua? Atachapisha picha zangu?' Hiyo ndiyo hofu inayowazuia kujilinda," anasema. Michelle pia anasema watu wazima bado humdharau kwa sababu ya umri wake. "Changamoto yangu kubwa imekuwa watu kudhani siwezi kuelewa masuala haya kwa sababu mimi ni msichana mdogo," anasema. Baada ya kumaliza shule ya upili, Michelle anapanga kusomea sheria ili kuongeza uwezo wake wa kushawishi sera zinazolinda watoto na vijana. "Nataka kuelewa sheria zinazowalinda watoto na kutumia taaluma hiyo kuleta mabadiliko makubwa zaidi," anasema.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.