WIRE โ€” IDARA ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imechukua rasmi uchunguzi wa madai ya wizi wa takriban Sh6.2 bilioni kupitia mfumo wa mishahara ya watumishi wa umma, baada ya Wizara ya Utumishi wa Umma kukabidhi ripoti za ukaguzi na uchunguzi wa kitaalamu zinazobainisha dosari kubwa katika mishahara serikalini. Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku pamoja na Katibu Jane Imbunya walikabidhi ripoti ya ukaguzi wa mfumo wa mishahara, ripoti 14 za uchunguzi wa kitaalamu na stakabadhi nyingine kwa Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin ili kuanzisha uchunguzi wa jinai. Ukaguzi huo uliofanywa katika idara 12 kati ya 53 za serikali uligundua ukiukaji mbalimbali unaoshukiwa kusababisha hasara ya Sh6.2 bilioni. Miongoni mwa dosari zilizobainika ni kubadilishwa kwa rekodi za mishahara bila idhini, malipo yasiyo halali ya mishahara, udhaifu katika usimamizi wa makato ya kisheria na mapengo makubwa katika mifumo ya usimamizi wa mishahara. "Leo nimekabidhi rasmi stakabadhi za ukaguzi wa mishahara kwa Mkurugenzi wa DCI. Hatua hii inaashiria kuanza kwa uchunguzi wa jinai kuhusu masuala yaliyobainika katika ripoti hiyo," alisema Bw Ruku baada ya kukutana na Bw Amin jijini Nairobi. Alisema madai yote ya ulaghai, matumizi mabaya ya afisi na ubadhirifu wa fedha yatachunguzwa kwa njia huru na utaalamu. Pia, aliwataka maafisa wa serikali za kitaifa na kaunti kushirikiana kikamilifu na wachunguzi ili ukweli ubainike. Hatua hiyo inafuatia agizo la Baraza la Mawaziri lililoongozwa na Rais William Ruto wiki iliyopita, lililoitaka DCI kuchunguza madai hayo na kuwafikisha mahakamani wote watakaopatikana na hatia. Baraza hilo pia liliagiza wachunguzi kuthibitisha nambari za utumishi zinazotumika katika mfumo wa mishahara, kuvunja mitandao ya wanaovuruga mfumo huo, kurejesha fedha za umma zilizopotea na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa. Hapo awali, Bw Ruku alikuwa ameonya kuhusu visa vya baadhi ya watumishi wa umma kupandishwa madaraja ya kazi na mishahara kinyume cha sheria ili wapate malipo makubwa. Alisema mamia ya maafisa wa serikali wanachunguzwa kwa madai ya kushirikiana katika ubadhirifu wa fedha za umma kupitia mfumo wa mishahara. Ukaguzi huo ulianza Desemba 2025 baada ya serikali kuunda timu ya mashirika mbalimbali iliyoongozwa na Idara ya Ujasusi (NIS), kufuatia hoja zilizotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu. Katika ripoti yake ya mwaka wa fedha uliomalizika Juni 2025, Bi Gathungu pia alibaini kuwa baadhi ya kaunti zilikuwa zikiwalipa mishahara na marupurupu watumishi wasiostahili, wakiwemo waliostaafu na waliokuwa wakipokea posho za ulemavu bila kutimiza vigezo vinavyofaa, hali iliyozua wasiwasi kuhusu usimamizi wa fedha za umma.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.