WIRE โ€” KWA miongo kadhaa, taswira ya mhuni wa kisiasa nchini Kenya ilikuwa ya kijana asiye na ajira, aliyevalia fulana ya chama cha kisiasa na kurushia mawe wapinzani kabla ya kutoweka kwenye umati. Wanawake walikuwa na nafasi tofauti. Waliimba nyimbo za kampeni, walicheza, walishangilia na kuhamasisha wapigakura na kwa nadra walihusishwa moja kwa moja na vitendo vya vurugu. Hata hivyo, hali hiyo inaonekana kubadilika katika baadhi ya maeneo ya Kisii. Baada ya msafara wa kisiasa wa Linda Mwananchi kuvamiwa huko Keumbu, katika eneo la Nyaribari Chache Ijumaa iliyopita, wachunguzi waliwakamata wanawake sita na mwanamume mmoja kuhusiana na tukio hilo. Shambulio hilo lilisababisha kifo cha mtu mmoja, majeraha kwa wengine kadhaa na uharibifu wa magari mengi, likiwemo lililombeba aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga. Kukamatwa kwa washukiwa hao kumeibua mjadala kuhusu mwenendo mpya ambapo wanawake wanadaiwa kushiriki kikamilifu katika makabiliano ya kisiasa badala ya kubaki pembeni. Macho mengi sasa yameelekezwa kwa kundi la Ebirongo, linalofanya shughuli zake katika maeneo ya Nyaribari Chache. Kundi hilo lilianzishwa kama kikosi cha kuhamasisha vijana, lakini wanachama wake wanasema baadaye lilipanuliwa na kujumuisha wanawake kwa lengo rasmi la kuimarisha uhamasishaji wa jamii na kuwawezesha wanawake. Wanawake kadhaa waliozungumza bila kutaka kutajwa majina walisema ugumu wa maisha ndio uliowasukuma kujiunga na uhuni. Mjane mmoja mwenye umri wa miaka 31 alisema: "Nilijiunga na Ebirongo Januari mwaka huu. Niliambiwa ni kazi ya kumuunga mkono mheshimiwa. Lakini ukifika uwanjani unaambiwa, 'Zuia huyu asiongee.' Ukikataa, hupati chochote siku inayofuata. Nina familia. Sh1,000 kwa siku ni fedha nzuri." Mwanamke mwingine alisema miezi mingi ya kukosa ajira ilimlazimu kukubali uhuni wa kisiasa. Baadhi yao pia wanaamini wanawake hawashukiwi haraka kama wanaume, jambo linalowarahisishia kuingia kwenye mikutano ya wapinzani bila kuzua wasiwasi. Vurugu hizo pia zimeathiri uchumi wa Keumbu, huku wafanyabiashara wakilalamikia kuporomoka kwa biashara baada ya baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii kutoa wito wa kususia bidhaa kutoka eneo hilo.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.