WIRE โ HUKU zikiwa zimesalia siku nane kabla ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ol Kalou utakaofanyika Julai 16, eneo hilo linashuhudia kampeni zinazotajwa kuwa miongoni mwa ghali zaidi katika historia ya Kaunti ya Nyandarua. Vyama vya United Democratic Alliance (UDA) na Democracy for the Citizens Party (DCP) vinaongoza kampeni hizo kwa kutumia mikakati mbalimbali ya kuwashawishi wapigakura. Mbali na mikutano ya kisiasa, wagombeaji na wafuasi wao wamekuwa wakigawa fedha, zawadi na kuandaa mikutano ya uhamasishaji huku serikali ikiendelea kuzindua miradi ya maendeleo katika eneo hilo. Kiti hicho kilibaki wazi baada ya kifo cha Mbunge Njuguna Kiaraho wa chama cha Jubilee, Machi 29, 2026. Wanaowania kiti hicho ni Kamau Ngotho wa DCP, Muchina Nyaga wa UDA, Wilson Kigwa wa Jubilee, Rachel Wangui wa People's Democratic Party, Mathenge Mwaniki wa Kenya Moja Movement, Abdifatah Hussein wa Federal Party of Kenya, Timothy Kamau wa People's Renaissance Party, Stephen Wanyoike wa National Liberal Party na Edwin Muchiri wa Party of National Unity. Kwa mujibu wa walio karibu na kampeni za DCP, makazi ya Seneta wa Nyandarua John Methu katika eneo la Mugumo yamegeuzwa kuwa kituo kikuu cha uratibu wa shughuli za chama hicho. [caption id="attachment_189921" align="alignnone" width="720"] Wakazi waliohudhuria mkutano wa kisiasa wapewa magodoro. Picha|Hisani[/caption] Kila asubuhi, makundi mbalimbali hukusanyika hapo kabla ya kutumwa katika maeneo tofauti kufanya kampeni. Washiriki hupewa kifungua kinywa na fedha za kujikimu zinazokadiriwa kuwa kati ya Sh500 na Sh1,000 kabla ya kuanza shughuli za siku. Akizungumza jana, kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua aliwataka wakazi wa Ol Kalou kutodanganywa na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali wakati huu wa kampeni. "Serikali inaweza kuleta hata boti, transfoma, treni za kasi, matangi ya maji pamoja na miradi mingine ambayo haijawahi kufikishwa Ol Kalou tangu 1963. Msikubali kuuza haki yenu ya kupiga kura kwa sababu ya zawadi za dakika za mwisho," alisema Bw Gachagua. Kwa upande wa UDA, kampeni zinaonekana kuwa na mtandao mpana zaidi. Chama hicho kimeunda timu mbalimbali zinazolenga makundi tofauti ya wapigakura huku washiriki wakipewa fedha za kujikimu kulingana na aina ya shughuli wanazoshiriki. Baadhi ya timu hizo husafirishwa hadi miji jirani kama Gilgil kwa mikutano ya kupanga mikakati, ambapo kila mshiriki hudaiwa kulipwa kati ya Sh1,000 na Sh2,000. Duru zenye ufahamu kuhusu kampeni hizo zinaeleza kuwa UDA huandaa wastani wa mikutano sita kila siku, huku viongozi wa serikali na waliochaguliwa wakihusika moja kwa moja katika shughuli hizo. Mbali na mikutano ya hadhara, chama hicho pia kimekuwa kikifanya mikutano na viongozi wa dini, wazee wa makanisa na waumini wenye ushawishi mkubwa, mikutano ambayo huwasilishwa kama warsha za amani na elimu ya uraia. Kiongozi mmoja wa kidini aliyeshiriki katika baadhi ya mikutano hiyo alisema kiwango cha fedha kinachotolewa hutegemea hadhi ya mkutano. Alidai kuwa mikutano ya kiwango cha kaunti washiriki hupokea takriban Sh5,000 kila mmoja huku mikutano ya ngazi ya mashinani wakipata karibu Sh3,000, bila kujumuisha fedha zinazotolewa kwa makanisa na viongozi wa dini wanaoratibu shughuli hizo. Kwa mujibu wa watu wanaofahamu mipango ya kampeni, mikutano mingi ya ndani huvutia takriban watu 500 wanaopewa kati ya Sh1,000 na Sh2,000 kila mmoja. Wanaoongoza kampeni pia hulipwa kati ya Sh5,000 na Sh10,000. Makadirio yanaonyesha kuwa UDA inaweza kutumia zaidi ya Sh3 milioni kwa siku kugharamia mikutano ya ndani pekee, bila kujumuisha gharama za usafiri, malazi, chakula na shughuli nyingine za kampeni. Baada ya mikutano ya hadhara, washiriki wengi huripotiwa kupanga foleni katika makundi ya watu kumi, utaratibu unaojulikana kama "ikumi ikumi", ambapo kila mmoja hupokea kati ya Sh300 na Sh500. Kutumiwa kwa fedha kumeibua biashara mpya kwa baadhi ya vijana wa eneo hilo. Makundi ya vijana hukodisha pikipiki kwa siku nzima na kuhama kutoka mkutano mmoja wa kampeni hadi mwingine ili kuongeza kiwango cha fedha wanachopata. Mwendesha bodaboda James Kanja alisema vijana watatu au wanne huchangia takriban Sh3,000 kukodisha pikipiki kwa siku pamoja na gharama ya mafuta. "Ni biashara nzuri kuliko kusubiri abiria mjini. Tunaweza kuhudhuria zaidi ya mikutano mitano kwa siku na kila mmoja akaondoka na kati ya Sh2,500 na Sh4,000," alisema. Mwendesha bodaboda mwingine, Robert Kiambati, alisema vijana hufuatilia ratiba za kampeni ili kujua mikutano inayotarajiwa kutoa fedha nyingi zaidi. Huku kampeni zikiendelea, serikali nayo imeongeza kasi ya kuzindua miradi ya maendeleo katika eneo hilo. Miradi hiyo ni pamoja na usambazaji wa mitungi 20,000 ya gesi, matangi ya maji, godoro, vyakula, vifaa vya kidijitali kwa shule za sekondari msingi, pamoja na boti mbili za thamani ya Sh5 milioni kwa Bwawa la Gwa Kiongo. Mawaziri na Makatibu mbalimbali wamekuwa wakizuru eneo hilo mara kwa mara kuzindua miradi ya barabara, umeme, nyumba za bei nafuu, masoko ya kisasa, reli na huduma za kidijitali. Kwa upande wa DCP, uchaguzi huo pia umegeuka kuwa uwanja wa kujitambulisha kwa wanasiasa wanaojiandaa kugombea viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Baadhi ya wanaotaka ugavana, ubunge na uwakilishi wa wadi wamekuwa wakifanya kampeni za nyumba kwa nyumba kwa gharama zao wenyewe ili kuongeza nafasi za mgombeaji wa DCP, Kamau Ngotho.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.