WIRE โ ILIKUWA hasara tele baada ya serikali kufunga baadhi ya barabara kuu zinazoingia Nairobi na kuimarisha usalama kuzima maandamano ya Saba Saba jana. Maelfu ya wasafiri walikwama asubuhi baada ya polisi kufunga kwa muda baadhi ya barabara kuu na kuzuia magari mengi ya uchukuzi wa umma kuingia jijini Nairobi. Hatua hiyo ilisababisha foleni ndefu za abiria katika vituo vya mabasi huku wengi wakishindwa kufika kazini, wafanyabiashara wakakosa wateja na shughuli nyingi za kiuchumi kusimama kutokana na ukaguzi mkali uliowekwa katika maeneo mbalimbali kwenye barabara za Thika, Jogoo, Mombasa na Waiyaki Way. Polisi waliweka vizuizi katika maeneo ya Kimbo, Kihunguro na makutano ya Barabara ya Eastern Bypass kwenye Barabara ya Thika, ambako walikuwa wakisimamisha na kukagua magari yaliyokuwa yakielekea Nairobi. Magari ya kibinafsi yaliruhusiwa kuendelea na safari baada ya kukaguliwa, lakini matatu nyingi zilizuiwa kuingia barabara hiyo, hali iliyowaacha mamia ya abiria bila usafiri. Kufungwa kwa baadhi ya sehemu za Barabara ya Thika na Mombasa Road pia kulisababisha msongamano mkubwa wa magari, huku matatu chache zilizohudumu zikikataa kuelekea katikati mwa jiji la Nairobi kwa kuhofia vizuizi vilivyowekwa na polisi. Maduka yalifungwa jijini huku shughuli za masomo zikitatizwa walimu wakiagiza wazazi kukaa na watoto wao nyumbani. Hata usafiri wa wanafunzi kwenda shule haungewezekana kutokana na vizuizi vilivyowekwa na polisi. Biashara nyingi hazikufunguliwa na hata zilizofunguliwa hazikupata wateja. "Nimekuwa hapa kwa saa mbili sasa na hakuna matatu. Zile chache zinazofika zinasema haziendi mjini," alisema Martin Oduor, mmoja wa wasafiri waliokwama katika kituo cha Githurai 45. Alisema hatua hiyo iliwaathiri zaidi watu wanaotegemea mapato ya kila siku ili kujikimu. "Inasikitisha sana. Wengi wetu tunaishi kwa kutegemea kile tunachopata kila siku. Lazima tufike kazini ili tupate riziki, lakini sasa polisi wametuzuia. Siwezi kufika kazini," alisema. Wasafiri wengi walionekana wakisubiri kando ya barabara wakitumaini kupata usafiri mbadala, huku wengine wakiamua kutembea kwa miguu umbali mrefu baada ya kubaini kuwa hawangeweza kupata matatu ya kuelekea jijini. Operesheni hiyo ya usalama ilijiri polisi wakiongeza ulinzi na kudhibiti njia za kuingia Nairobi kabla ya maandamano ya Saba Saba, huku maafisa wa usalama wakimwagwa kwa wingi katika barabara kuu zinazoelekea katika mji mkuu. Hali ilikuwa tulivu katika eneo la Mlolongo kwenye Barabara ya Mombasa licha ya uwepo mkubwa wa maafisa wa polisi waliokuwa kwenye doria kabla ya maandamano hayo. Maafisa wa polisi walikuwa wamepiga kambi katika lango la kuingia na kutoka Barabara ya Expressway eneo la Mlolongo, lakini tofauti na ilivyokuwa Juni 25 wakati wa kumbukumbu ya miaka miwili ya maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024, hakukuwa na vizuizi vikubwa barabarani. Siku hiyo ya Juni 25, polisi walikuwa wakikagua kwa makini magari yote yaliyokuwa yakitaka kupita eneo hilo, huku madereva wengi wakielekezwa kurejea walikotoka. Hata hivyo, jana hakukuwa na vizuizi katika sehemu kubwa ya Barabara ya Mombasa isipokuwa katika mzunguko wa Barabara ya Bunyala, ambako maafisa walikuwa wakikagua baadhi ya magari yaliyokuwa yakielekea katikati mwa jiji. Maafisa wengine walionekana wakishika doria katika maeneo mbalimbali, yakiwemo lango la Expressway Mlolongo, makutano ya Mlolongo na Kitengela, mzunguko wa Barabara ya Bunyala pamoja na makutano ya Barabara ya Haile Selassie na Uhuru Highway. Licha ya uwepo huo wa polisi, shughuli za usafiri ziliendelea kwa utulivu huku msongamano wa magari ukiwa mdogo kuliko ilivyo kawaida kwenye Barabara ya Mombasa. Wakati huo huo, kiongozi wa Chama cha People's Liberation Party (PLP), Martha Karua, alikosoa hatua ya serikali ya kufunga baadhi ya barabara nchini. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi ya chama hicho katika eneo la Nyamataro, Kaunti ya Kisii, Bi Karua alisema Wakenya hawapaswi kuzuiwa kutoa maoni yao au kutumia haki zao za kikatiba mradi wanafanya hivyo kwa amani. "Serikali haipaswi kuweka vizuizi vya barabarani kama ilivyofanya leo katika maeneo mbalimbali nchini. Ni jambo la kusikitisha. Tulinde amani huku tukiheshimu haki na uhuru wa wananchi," alisema. Kaunti ya Embu nayo ilishuhudia taharuki huku polisi wa kutuliza ghasia waliokuwa wamejihami kwa silaha wakishika doria mjini humo kabla ya maandamano ya Saba Saba. Maafisa hao walionekana wakizunguka katika mitaa mbalimbali huku wafanyabiashara wengi wakiendelea na shughuli zao kama kawaida. Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara hawakufungua maduka yao asubuhi kwa hofu kwamba huenda maandamano yangesababisha vurugu. Katika Barabara Kuu ya Embu-Makutano, polisi waliweka vizuizi na kuwakagua madereva pamoja na magari yaliyokuwa yakitumia njia hiyo ili kuhakikisha hayakusafirisha wahuni waliokusudia kuvuruga amani. Ukaguzi huo ulisababisha msongamano wa magari katika barabara hiyo ambayo kwa kawaida huwa na shughuli nyingi. Aidha, wasafiri waliokuwa wakielekea Nairobi walikwama katika kituo cha mabasi cha Embu baada ya wahudumu wa matatu kususia safari kuelekea mji mkuu kwa kuhofia hali ya usalama. Baadhi ya wasafiri hao walilazimika kukatiza safari zao na kurejea nyumbani baada ya kubaini hawangeweza kupata usafiri wa kuelekea Nairobi.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.