WIRE โ€” MUUNGANO wa upinzani umeangukiwa na mizimwi ya dhiki chungu nzima za kisiasa. Muungano huo umeendelea kubanwa katika kuandaa mikutano huru kwa kushambuliwa na wahuni mara kwa mara, viongozi katika upinzani nao wanajikanganya kwa kukosa kusema kwa kauli moja. Kila mmoja wao anahema kwa kishindo akitaka kuwa mgombea urais. Ingawa viongozi hao wanatangaza umoja katika kampeni zao wakati wa mchana, baadhi yao kama Caleb Amisi wamekosa imani na mrengo wa Linda Mwananchi na kujiunga na Chama cha PRM. Huenda Amisi ametabiri kusambaratishwa kwa mrengo huo na chamchela ya tamaa za viongozi wa upinzani. Kuna migogoro ya ndani kwa ndani katika upinzani na huenda hivi karibuni nyufa katika muungano huo zikaongezeka na upinzani kulemazwa zaidi kisiasa. Viongozi katika muungano huo hawana msimamo mmoja. Rigathi Gachagua anahisi kuwa mwaniaji wa urais wa muungano huo anafaa kutajwa uchaguzi unapokaribia huku Justin Muturi akitaka uteuzi ufanyike mapema. Ni nani wa kuaminika? Sifuna amepata nguvu mpya kutoka kwa viongozi wa Magharibi kuwania urais huku Kalonzo Musyoka akionekana bora zaidi kuchukua nafasi hiyo. Kenya Kwanza nayo imenoa makali yake na kujaribu kufuta nyayo za upinzani katika maeneo yaliyoonekana kushabikia upinzani. Kwanza, wapo viongozi wa Kenya Kwanza wanaoendelea kujitolea kushabikia serikali ukanda wa mlima Kenya uliodhaniwa kuwa ngome ya chama cha DCP. Moses Kuria, Kimani Ichungwa, Anne Waiguru na wengine wamebaki kupigia upatu awamu ya pili ya serikali ya UDA. Hii inasambaratisha kufaulu kwa upinzani kwani eneo hilo halina ari kubwa ya kuwa na mgombea wa urais. Siasa za kuwa uwepo wa Mlima Kenya Mashariki na Magharibi zimetokota. Kundi la Mashariki likishinikizwa kujiona tofauti na lile la Magharibi ili uzuia wananchi hao kushirikiana katika kufanya uamuzi wa kupiga kura. Hali hii itauzuia upinzani kunyakua kura nyingi hivyo kupiga jeki kapu la kura la UDA. Kufikia sasa, upinzani haujaweza kushirikiana kubuni sera za kuuongoza ili kuonyesha mshikamano wao. Kutia chumvi kwenye kidonda ni kuwa kuna kundi la Linda Mwananchi lililoonekana kushika kasi kisiasa na kutaka kujisimamia kisiasa. Hili litakuwa pigo kubwa katika muungano wa upinzani. Kuondoka kwa Caleb Amisi kutoka Linda Mwananchi huenda ukawa mwanzo wa kuyumba kwa upinzani. Viongozi na vyama vingine katika Linda Mwananchi bado wanasoma dalili na pengine watajiunga na Kenya kwanza kwa kuogopa kupigwa na baridi ya kisiasa kwani nguvu za upinzani huenda zikazidi kuwa hafifu na kufanya wakose kuchaguliwa katika maeneo yao. Ushabiki uliokuwepo wa vijana katika upinzani pia umepoa hivyo vijana huenda wanasubiri mwamko mpya wa kuwapa hamasa za kupiga kura. Kangai ni mwalimu na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.