WIRE โ MSAJILI Mkuu wa Ardhi yuko hatarini kukamatwa baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi kumpata na hatia ya kuidharau kwa kukosa kutekeleza amri iliyotolewa katika mzozo wa ardhi unaowahusisha aliyekuwa Mama wa Taifa Mama Ngina Kenyatta na mfanyabiashara Basil Criticos. Katika uamuzi mkali unaosisitiza kuwa mahakama haitavumilia ukaidi wa kutotekeleza maagizo yake, Jaji C.G. Mbogo amemwamuru Msajili Mkuu wa Ardhi afike binafsi mahakamani Julai 28, 2026, kueleza ni kwa nini asichukuliwe hatua kwa kukaidi hukumu iliyotolewa zaidi ya miezi sita iliyopita. Jaji alionya kuwa ikiwa msajili huyo hatajitokeza mahakamani, kibali cha kukamatwa kwake kitatolewa. Uamuzi huo unatokana na mzozo wa muda mrefu kuhusu umiliki wa ardhi, ambapo mahakama ilibaini kuwa Ofisi ya Usajili wa Ardhi ilishindwa kutekeleza hukumu iliyotolewa Desemba 11, 2025, licha ya kukumbushwa mara kadhaa na mwenye amri hiyo ya mahakama. Ombi hilo liliwasilishwa na mfanyabiashara Basil Criticos aliyedai kuwa Msajili Mkuu wa Ardhi amekuwa akikwamisha utekelezaji wa hukumu kwa kukataa kutoa cheti cha muda cha umiliki wa ardhi hiyo yenye utata. Kwa mujibu wa stakabadhi za mahakama, msajili alikumbushwa kupitia barua mnamo Desemba 17, 2025 na Januari 13, 2026, huku hukumu hiyo ikisajiliwa rasmi dhidi ya hati ya ardhi Januari 22, 2026. Hata hivyo, hakuna hatua iliyochukuliwa. Akiwa amechoshwa na kucheleweshwa huko, Bw Criticos alirejea mahakamani akiomba msajili alazimishwe kueleza sababu za kutotekeleza amri ya mahakama na pia achapishe katika Gazeti Rasmi la Serikali taarifa ya kufutwa kwa hati zote za ardhi zilizotolewa kinyume cha sheria kutokana na ardhi hiyo. Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Ardhi alijitetea kupitia hati iliyowasilishwa na afisa wa usajili wa ardhi Nyandoro David Nyambaso. Alieleza kuwa cheti cha muda cha umiliki tayari kilikuwa kimeandaliwa lakini hakikuweza kutolewa baada ya kugundua hitilafu katika stakabadhi za kuhamisha ardhi. Kwa mujibu wa kiapo hicho, hati ya kuhamisha ardhi ilishuhudiwa na D.A. Gama Ross ambaye sasa ni marehemu, jambo ambalo lilihitaji ufafanuzi kabla ya usajili kuendelea. Msajili huyo pia alidai kuwa ardhi hiyo tayari ilikuwa imepimwa, kupangwa na kugawiwa wavamizi waliokuwa wakisubiri kupewa hati miliki, akisema kuwa kufuta hati hizo kupitia Gazeti Rasmi bila kufuata utaratibu wa kisheria kungekuwa kinyume cha sheria. Hata hivyo, Jaji Mbogo alitupilia mbali hoja hizo akisema ztayari zilijadiliwa kabla ya hukumu kutolewa, hivyo haziwezi kutumiwa kuhalalisha kutotekelezwa kwa amri za mahakama. Jaji alikubaliana na Bw Criticos kwamba msajili alikuwa akijaribu kufufua hoja ambazo tayari zilikuwa zimeamuliwa na mahakama na akabaini kuwa hakuna shaka kuwa Msajili Mkuu wa Ardhi anafahamu amri ya mahakama lakini alichagua kutotii.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.