WIRE โ€” MAHAKAMA Kuu imeamuru Dayosisi ya Eldoret ya Kanisa Katoliki kumjumuisha mwanamume anayedaiwa kuzaliwa na Padri aliyefariki katika ugavi wa mali yake, ikisema watoto wote wana haki ya kurithi wazazi wao bila kujali mazingira ya kuzaliwa kwao. Jaji Reuben Nyakundi aliamua kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulithibitisha kuwa DK, aliyezaliwa Julai 4, 2003, ni mtoto wa kibaolojia wa marehemu padri JKN, aliyefariki Julai 2015. Kabla ya kifo chake, kasisi huyo alikuwa amemteua Askofu Cornelius Korir kuwa msimamizi wa wosia wake. Hata hivyo, Askofu Korir alifariki mwaka 2017 kabla ya kukamilisha usimamizi wa mali hiyo, na nafasi yake ikachukuliwa na Askofu Dominic Kimengich. Mchakato wa ugavi wa mali ulichukua mkondo mpya baada ya mama wa DK, NJR, kupinga kuondolewa kwa mwanawe kwenye orodha ya warithi. Wasimamizi wa mali hiyo walipinga ombi hilo wakidai kuwa Padri JKN alikuwa kasisi aliyekuwa ameweka nadhiri ya useja, hivyo asingeweza kupata mtoto. Lakini Jaji Nyakundi alisema cheti cha kuzaliwa cha DK, kinachomtaja marehemu kuwa babake, pamoja na ushahidi wa mama yake, vilitosha kuthibitisha kwa kiwango kinachohitajika katika kesi ya aina hiyo. "Ni wazi kuwa mali ya marehemu haiwezi kumfanya DK kuwa mtoto asiye na haki kwa kukosa kumtengea sehemu ya urithi wa marehemu," alisema jaji. Mahakama pia ilitangaza kuwa cheti cha kuzaliwa kilichotolewa Machi 12, 2008 kinamtambua marehemu kuwa baba wa mtoto huyo. Katika uamuzi wake, Jaji Nyakundi alisema watoto waliozaliwa nje ya ndoa ni warithi halali wa mali ya wazazi wao na kwamba wosia hauwezi kutumiwa kunyima watoto hao haki zao za kikatiba. "Watoto waliozaliwa kutokana na mahusiano kama hayo wana haki ya kurithi mali ya wazazi wao, iwe ni mali inayohamishika au isiyohamishika, na hakuna wosia unaoweza kutumika kuwanyima haki hizo," alisema. Mahakama iliwapa wasimamizi wa mali siku 60 kumgawia DK sehemu yake ya urithi, ikionya kuwa wakishindwa kufanya hivyo, hati ya usimamizi wa mali itafutwa na mchakato mpya wa urithi utaanzishwa. Jaji pia alikataa ombi la kufukua mwili wa kasisi huyo kwa uchunguzi wa vinasaba (DNA), akisema hatua hiyo ingeingilia haki za faragha za watu wengine bila sababu ya msingi. Katika ushahidi wake, NJR alisema alikutana na Padri JKN mwaka 1993 alipokuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi. Alidai uhusiano wao ulianza kama wa ushauri kabla ya kuwa wa kimapenzi, na kwamba kasisi huyo alimsaidia kielimu, kumpatia kazi na kugharamia mahitaji ya mtoto wao, ikiwemo karo, kodi ya nyumba na matumizi mengine. Jaji alisema upande uliopinga madai hayo haukuwasilisha ushahidi wa moja kwa moja wa kupinga uhusiano huo.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.