WIRE โ€” SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna anatarajiwa kuongoza wimbi la viongozi kujiondoa katika chama cha ODM baada ya viongozi wa jamii ya Waluhya wanaohusishwa na mrengo wa Linda Mwananchi kukubaliana kumpigia debe kuwania urais mwaka wa 2027 kupitia chama kipya cha kisiasa. Uamuzi huo ulifikiwa Jumapili katika mkutano ulioandaliwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, ukiwaleta pamoja Bw Sifuna, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, Mbunge wa Bumula Wamboka Wanami pamoja na viongozi wengine. Viongozi hao walitangaza kuwa wako katika hatua za mwisho za kuunda chama kipya watakachotumia katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027. Hatua hiyo pia inaonekana kufungua ukurasa mpya kwa Bw Sifuna ambaye kwa sasa anakabiliwa na mzozo wa kisheria kuhusu wadhifa wake kama Katibu Mkuu wa ODM. Akizungumza baada ya mkutano huo, Seneta Osotsi alisema bado wanazingatia uwezekano wa kutumia jina Linda Mwananchi licha ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kukataa ombi lao la usajili mwezi Machi mwaka huu kwa msingi kuwa jina hilo linafanana na kauli-mbiu iliyopo tayari na hivyo kukiuka Sheria ya Vyama vya Kisiasa. Alisema iwapo wataamua kuendelea na jina hilo, hawatakuwa na budi ila kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Kisiasa mahakamani wakisisitiza kuwa haukujikita katika msingi wa kisheria. Bw Osotsi alieleza kuwa chama hicho hakitakuwa cha viongozi wa Magharibi pekee bali kitawaleta pamoja viongozi wote wanaohusishwa na mrengo wa Linda Mwananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini. Viongozi hao wamepanga kufanya mikutano miwili mikubwa ya kisiasa katika kaunti za Trans Nzoia na Bungoma mnamo Julai 25 na 26, mtawalia. Mikutano hiyo itatumika kuzindua rasmi mkakati wao wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 pamoja na kuanza kampeni za mashinani katika maeneo yote 38 ya uchaguzi ya eneo la Magharibi. Katika mkutano wa Bungoma, Bw Sifuna anatarajiwa kutawazwa rasmi kuwa kinara wa kisiasa wa eneo la Magharibi na kupewa baraka za wazee kuwania urais. "Azimio letu ni kwamba Bw Sifuna atagombea urais mwaka wa 2027. Hivi karibuni tutatangaza chama tutakachotumia kuwania urais," alisema Bw Natembeya. Aliongeza kuwa viongozi hao wataanzisha kampeni kali za kuwahamasisha wananchi kujisajili kama wapigakura na kuunga mkono ajenda yao ya kisiasa. Kwa upande wake, Bw Osotsi alisema eneo la Magharibi limeendelea kugawanyika kisiasa kwa manufaa ya viongozi kutoka maeneo mengine, akisisitiza kuwa wakati umefika kwa wakazi wa eneo hilo kupigania kiti cha juu zaidi ya uongozi nchini. Mrengo wa Linda Mwananchi pia unajumuisha viongozi wengine mashuhuri akiwemo Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi, Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Anthony Kibagendi, Mbunge wa Kitutu Masaba Clive Gisairo, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Mbunge wa Kaiti Joshua Kimilu na Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata. Bw Natembeya alisema kwa sasa anaendelea kuwa mratibu wa kisiasa wa mrengo wa Linda Mwananchi na pia muungano wa upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pamoja na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika eneo la Magharibi. Hata hivyo, Bw Osotsi alisema Bw Natembeya anatarajiwa kutangaza rasmi kujiunga na mrengo wa Linda Mwananchi wakati wa mkutano wa Julai 25. Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alisema iwapo hawatafaulu kusajili chama kipya kwa muda uliosalia kabla ya uchaguzi mkuu, watanunua chama ambacho tayari kimesajiliwa ili kitumike kama chombo chao cha kisiasa. Alisema uamuzi wao wa kujiondoa ODM umetokana na tofauti za kisiasa na kundi linaloongozwa na Oburu Oginga, ambalo limejitokeza kumuunga Rais William Ruto kuwania muhula wa pili. Wakati huo huo, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amethibitisha kuwa ana uhusiano na chama kipya cha United Patriotic Movement (UPM), ambacho tayari kimekidhi masharti ya usajili na kinasubiri usajili kamili. Alisema UPM ni chama cha kitaifa kitakachowaleta pamoja viongozi wanaotaka kuona Rais Ruto akihudumu kwa muhula mmoja pekee, akiongeza kuwa taarifa rasmi kuhusu iwapo kitakuwa chombo kipya cha viongozi wa Linda Mwananchi itatolewa katika wiki zijazo. Hatua hizi zinaashiria kuanza kwa mabadiliko makubwa ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, huku vyama vikuu vikitarajiwa kupoteza baadhi ya viongozi wao wanaotafuta vyama vipya vya kisiasa vya kuwania nyadhifa mbalimbali.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.