WIRE โ€” HII leo, dunia nzima inaadhimisha makala ya tano ya Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU), tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) litoe tangazo mnamo mwaka wa 2021, kutambua na kuthibitisha Kiswahili kuwa lugha yenye umuhimu mkubwa duniani katika mazingira ya wingi-lugha. Kiswahili na lugha nyingine ni amali, rasilimali na nyenzo zinazohitaji kutunzwa na kukuzwa kwa ajili ya maendeleo. Kwa sababu hiyo, wataalamu wanaelekea kukubaliana kwamba mojawapo ya mikabala ya kuziangalia lugha ni ule wa kutoziona kama nyenzo za mawasiliano tu, bali pia kama bidhaa au rasilimali. Je, Afrika Mashariki imejinufaisha vipi kutokana na ubidhaishaji wa Kiswahili? Dunia inapokisherehekea Kiswahili, Afrika ya Mashariki inapaswa kuwa kwenye mstari wa mbele katika utetezi wa lugha hii, na utamaduni wake kwa minajili ya kujinufaisha kiuchumi. Tunapochunguza masuala ya siasa za kijiografia za lugha (geopolitics of languages), inabainika bayana kwamba mataifa mengine ulimwenguni yamebidhaaisha lugha zao kwa njia na namna mbalimbali. Kwanza, mataifa hayo yametumia lugha zao kufaidi kwenye masuala ya kidiplomasia na ushawishi (soft power influence). Je, tumewahi kujiuliza ni kwa nini Wachina wameanzisha taasisi kama vile Confucius Institute katika Vyuo Vikuu vya Nairobi na Kenyatta? Ni kwa nini Wafaransa wana Alliance Francais jijini Nairobi? Je, ni kwa nini Wajerumani wamestawisha Goethe Institute jijini Nairobi? Je, ni kwa nini Waingereza wamestawisha na kuimarisha shirika la Uchapishaji la Oxford University Press kote duniani? Je, maswali haya yanafungamana vipi na jinsi Afrika Mashariki (kitovu cha Kiswahili) inavyokishughulikia na kukiahangaikia Kiswahili? Si jambo la mjadala tena kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya kutazamwa sana barani Afrika, kuliko lugha nyingine kuu za bara hili. Afrika ya Mashariki ina bahati kubwa kuwa na Kiswahili, ambacho ni mojawapo ya rasilimali muhimu ya eneo hili. Si lazima rasilimali ziwe mafuta, almasi, na misitu pekee. Idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili kote ulimwenguni inakisiwa kuwa baina ya watu milioni 150 na 250. Wengi wa wazungumzaji hawa ni wenyeji wa Afrika ya Mashariki na Kati na Maeneo ya Maziwa Makuu. Ingawa Kiswahili ni lingua franca ya Afrika Mashariki, wasemaji asilia (watu wanaozungumza Kiswahili kama lugha yao ya 'mama' ni kati ya milioni 5 na 15. Fasihi simulizi inadokeza kwamba Waswahili walitoka sehemu za kaskazini ya pwani ya Kenya โ€“ mahali panapoitwa Shungwaya karibu na mji wa Lamu. Kutoka mahali hapa, walihamia sehemu nyingine za pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu ya vita, njaa, magonjwa n.k. Waswahili asilia (kindakindaki), chambacho mtaalamu Ireri Mbaabu waliitwa Wangozi na walizungumza Kingozi. Hili ni jina la lakabu lililotokana na vitendo vyao vya kupima ardhi kwa kutumia kanda za ngozi. Jina 'Waswahili' ama lilitokana na 'Wa- ziwa โ€“hili' (watu wa ziwa hili) au asili ya Kiarabu 'Sahil' (umoja) na 'Sawahil' (wingi) kwa maana ya watu wa pwani. Mbaabu anadai kuwa neno 'Kiswahili' lilianza kutumika sehemu ya kaskazini mwa pwani karibu na mji wa Lamu kati ya mwaka wa 700 โ€“ 800 Baada ya Yesu Kristo. Hii leo, Kiswahili si lugha ya pwani tu. Imekwisha kupasua kingo zake na kuenea katika sehemu mbalimbali ulimwenguni โ€“ na kupanua mawanda na maana 'Mswahili', jinsi inavyofahamika. Kuna takriban makundi manne ya 'Waswahili'. Kwanza, ni Waswahili wenye asili ya Kibantu. Pili, tuna Waswahili waliozaliwa kutokana na ndoa kati ya Waarabu na Waswahili asili (kindakindaki). Tatu, ni 'Waswahili' wanaotoka katika makabila mengine ya Kiafrika ambao wanashabikia na kuuenzi utamaduni wa Mswahili. Mwisho, kuna kundi la watu wanaoenzi na kuishughulikia lugha ya Kiswahili katika ulingo wa taaluma. Nilivyokwisha kutaja, Kiswahili ndiyo lugha ya kutazamwa barani Afrika karne hii. Ramani ya lugha inaonesha kwamba Kiswahili ni mojawapo ya lugha kumi na moja zenye wazungumzaji wengi zaidi barani Afrika. Kiswahili ndicho kinashikilia nafasi ya kwanza kwa kuwa na takribani zaidi ya wazungumzaji milioni 150 barani Afrika (wengi wao wakiwa wenyeji wa Afrika Mashariki). Lugha nyingine Afrika zenye wasemaji wengi ni Amharic, Kioromo , pamoja na Kiarabu (Afrika kaskazini). Katika Afrika ya Magharibi, tuna Kiyoruba na Igbo. Katika eneo la Afrika ya Kusini tuna Kizulu na Kishona. Kati ya lugha hizi zote, Kiswahili kimeungwa mkono na wataalamu wengi kuwa lingua franca ya Afrika. Kutokana na umaarufu wa Kiswahili, mataifa ya Afrika Mashariki yanapaswa kuimarisha uundaji na utekelezaji wa sera murua zitakazofanikisha michakato ya ubidhaishaji wake kwa minajili ya kujitajirisha kiuchumi โ€“ yanavyofanya mataifa mengine kuhusu lugha zao. Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.